JE, KWA NINI KISWAHILI KIFUNDISHWE MAREKANI?

Miezi kadhaa iliyopita nilihojiwa kuhusu ajira huku Marekani katika kufundisha Kiswahili.  Kwa sababu ninakipenda Kiswahili pamoja na nia ya kukichangia kikue popote kilipo nikafafanua mkakati wa kumpatia kazi Mtanzania anayetafuta ajira hiyo.

Kabla ya hapo mnamo mwaka wa 2007 niliwahi kwenda Tanzania kwa ajili ya kongamano, Dar es Salama.  Baada ya kutoa yangu kuhusu tabia mbaya ya kuchanganya lugha mbili maksudi katika kauli moja katika mpango wa kutumia Kiswahili kama chombo chenye kukibeba Kiingereza na maringo yanayokuja nayo, nikahojiwa tena.

Safari hii mhoji alikuwa msichana nakiri katika miaka ya kwanza ya chuo kikuu.  Mazungumzo yetu yakiwa katika Kiingereza yakawa kama haya yafuatayo:  Akaniomba niseme machache juu ya wavulana Watanzania na Kiswahili.  Nikamwuliza. “Je, katika waandishi mashuhuri wa Kiswahili nani anapendeza zaidi kwako?”   Bila ya kusita akajibu, “Shaaban Robert!”  Akaendelea.  “Kitabu chake, “Kufikirika”  kilikuwa kizuri sana pamoja na msamiati mgumu!”  “Sawa!”  Nikajibu.  “Lakini hicho ni kimoja tu katika mfululizo wa vitabu vyapata kumi na vitano hivi.   Kipi kingine kimekufurahisha?”  Sikupata  jibu.  Nikaendelea.  “Nadhani “Kufikirika” kinatakiwa shuleni au sicho?”   “Ndicho.”  Nikaendelea.  “Basi isitoshe Marehemu Shabaan alifariki dunia kiasi cha miaka sitini iliyopita!  Nani amemfuata kwa umashuhuri, na muhimu akipendeza kwako?”  Sikupata jibu.

Baada ya mazungumzo hayo nilienda duka la vitabu kununua kitakachonivutia.  Cha umuhimu sana kwangu kilikuwa kitabu nambari kumi katika mfululizo uitwao DIWANI YA SHAABAN nacho kinaitwa “Mashairi ya Shaaban Robert.” Sababu ya umuhimu wake ni ndicho kinachokosekana maktabani mwangu katika vitabu vya Marehemu Shaaban.  Kumbe!  Licha ya hicho kutopatikana vilivyokuwepo vilikuwa viwili tu!  Viwili vya mbobezi asiye na kifani katika historia ya Kiswahili!  Halafu nikamwulizia Marehemu Ben Mtoba ambaye ameandika riwaya zapata saba hivi zenye kusisimua na kubainisha mifano ya ufisadi angalau za kubuniwa.

Pamoja navyo alikiandika kimoja kuhusu harakati za Mhehsimiwa Rais Jakaya Khalfan Mrisho Kikwete kugombea na kuchagulia kuwa Rais wa Tanzania.   Nacho kinaitwa Safari ya Ikulu.  Ametoa mchango muhimu akiwa  mfano wa msomi na mtungaji aliyeshika wadhifa wa kuondoa ufisadi Tanzania.   Hesabu kwa mara ya pili ilikuwa viwili.

Sasa sijui Kiswahili kinaenda wapi Tanzania?  Na kama swali hilo linafaa kuulizwa swali linalofuata ni: Je, kwa nini Kiswahili kifundishwe Marekani?  Kiongozi kipofu wafuasi  wake hujikwaa wakizunguka zunguka mwendo wa magamaga!

Vinginevyo sina budi kurudia historia ya Marekani ilimradi tofauti baina ya Marekani na nchi za Ulaya zidhihirishwe, na kimsingi kueleza kwa nini Kiswahili kikapata umuhimu na kutokana na umuhimu huo kikapatia Watanzania pamoja na Wakenya ajira kwenye enzi za 1960 pamoja na 1970.  Wazazi wetu waliotekwa nyara Afrika Magharibi waliletwa ughaibuni katika sehemu za mabara mawili pamoja na visiwa vya Marekani wawe watumwa.

Mamilioni walitekwa wakiwa pamoja na wale waliokufa ama katika Afrika au kwenye Bahari ya Atlantiki.  Wachache sana walipelekwa nchi za Ulaya kutokana na ukosefu wa ardhi na hofu ya Wazungu kutochanganyika na Waafrika.  Lugha, mila, desturi, hata majina yalifutwa lakini sio kabisa.  Kwetu Umoja wa Majimbo ya Marekani, mdundo wa Kiafrika bado unasikika.  Halafu kwenye visiwa kama kwa mfano Jamaica, na Cuba pamoja na Brazil ambavyo viko kwenye bara la Marekani ya Kusini, lugha ya Kiyoruba bado inasikika na mila na desturi fulani kama kwa mfano dini ya Kiyoruba inaendelea na kudumu.

Kiswahili kikiwa lugha isiyo na msingi wa kikabila kikavutia sana kwenye enzi za 1960 na 1970 katika mapinduzi ya kiutamaduni hasa katika taifa letu la Umoja wa Majimbo ya Marekani.  Jambo hilo lilikuwa muhimu zaidi kuliko jambo la asili yetu iko wapi Afrika.  Kitovu cha umuhimu wa Kiswahili kikawa Tanzania kutokana na maadili ya harakati zake, kwanza kupata uhuru kisha kujenga taifa linalosisitiza maadili endelevu yakiwa na heshima kwa mila na desturi za Kiafrika.

Siku hizi harakati hizo zimepunguka katika mipango ya maisha ya vijana wa Marekani pamoja na wa Tanzania.  Kutokana na upungufu huu umuhimu wa Kiswahili umepungua Marekani pamoja na Tanzania.  Lengo langu katika kuandika makala haya ni kuwabainishia vijana kwanza halafu Watanzania wengine matokeo mengine ya upungufu wa umuhimu wa Kiswahili.

Siku hizi uchumi wa Tanzania unabadilika katika mfumo kutoka kwa mfumo wa umiliki wa serikali kwenda umiliki wa watu binafsi.  Sasa ni wajibu wa watoaji wa vitu pamoja na aina kadhaa za huduma kupima thamani ya bidhaa zao kutoka kwa upande wa wateja wakiwa  pamoja na wale wanaotarajiwa wawe wateja.  Mtoaji ni mwuzaji wa kwanza katika mkakati unaobadilishana kitu au huduma kwa pesa za bei yake.  Mwalimu ye yote yule ni mwuzaji mwanzilishi.  Ni kazi yake kufundisha thamani ya somo fulani kwa wanafunzi wake ilimradi wajue somo lenyewe litawafaidisha namna gani.

Kiswahili kikiwa lugha kinashindana na lugha nyinginezo kuvutia fursa ya kufundishwa,  mwalimu kuajiriwa, nafasi katika bajeti, n.k. Ninavyofafanua sasa ni kanuni ya soko huria.  Ninatoa mtihani kwa Watanzania kujadili changamoto za soko huria.  Kujiuliza, je, tunauza kitu gani?  Kwa nini tunakiuza hichi na hicho?  Kuzingatia kosa la kudhani pesa za mteja ni sababu ya kuuza kitu huku ukijiepusha na haja zake, sababu zake, mahitaji yake mteja, ama mtumiaji wa kitu husika badala ya mnunuzi mwenyewe.

Naomba mufikirie nchi tajiri na sifa za bidhaa zao.  Mifano ni Ujerumani na Mercedes Benz, Japani na Sony, Umoja wa Majimbo ya Marekani na John Deere.   Sifa za mifano hiyo ni matokeo ya kujiheshimu kwa walioanzisha utengenezaji wa bidhaa hizo.  Walianza kazi wakiwa na maadili ya kuumba na kutengeneza kwa kadiri kustahili kuwa waungwana.   Kwanza wawe waungwana halafu matajiri.

Mfano maalum ni kijana Mmalawi kwa jina anaitwa William Kamkwamba aliyejenga kinu cha upepo (windmill)  kutokana na takataka alipokuwa na umri wa miaka kumi na minne.   Sasa ana umri wa miaka ishirini na miwili. Habari zake zimesambazwa dunia nzima mathalan kitabu kiitwacho The Boy Who Hammered the Wind kuandikwa juu yake.  Mimi nilisoma habari zake katika gazeti la Los Angeles Times, makala yaitwao The Lost Art of Building With Your Hands.  Yeye amekuwa mfano wa akili timamu kwa watoto pamoja na vijana wa taifa hili kwa sababu alitumia akili zake, mikono yake na chochote kile kwa lengo la kuleta nishati nyumbani kwao.  Matokeo yake yalikuwa taa ya umeme.  Sasa wataalamu wa nishati wa nchi zote tajiri wanalitambua jina lake.

Madhumuni ya makala haya ni kutoa changamoto kwa vijana Watanzania kujenga Kiswahili kiwe chombo cha mawasiliano yanayowasilisha ujenzi wa vitu vya kisasa vikiwa na huduma za ukarimu unaojulikana dunia nzima kama sifa ya Tanzania.

Halafu huenda ajira katika kufundisha Kiswahili itarudi Marekani ikithibitishwa na umuhimu wa Kiswahili kuboreka Tanzania.

Asanteni    Profesa Mstaafu Pete M. Mhunzi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s