WANGEFELI KAMA WANGEJIBU KISWAHILI?

TUJIULIZE, WANGEFELI KAMA WANGEJIBU KISWAHILI?

KUTOKA CHINA

Njonjo Mfaume

NIMEJIKUTA katika mjadala mkali na mke wangu baada ya kumuuliza lugha gani angependelea itumike kufundishia kutoka shule za msingi hadi chuo kikuu. Yeye anapenda Kiingereza.

Anaamini ni vizuri kutumia Kiingereza kwa sababu ni lugha ya kimataifa inayotumika duniani kote na hivyo basi ni rahisi kwa muhitimu ‘kujichanganya’ kokote ulimwenguni kutafuta elimu zaidi au ajira.  Niliulizwa: “Sasa wakisoma kwa Kiswahili wakienda huko nje kuendelea kusoma itakuwaje”.

Nikaambiwa pia kwamba Kiswahili hakina vitabu vinavyoweza kutumika kufundishia katika ngazi mbalimbali za elimu na pia hakina misamiati ya kitaalamu ya nyanja na kada mbalimbali.

Sababu nyingine iliyotajwa ni kuwa Kiswahili hakina soko katika ajira, hata za ndani ya nchi, kwa maana ya kwamba waajiri wanahitaji watu wanaojua Kiingereza. Kwa maana hiyo wahitimu wasiojua Kiingereza watakuwa hawaajiriki, hususan, katika sekta binafsi.

Kimsingi, sitofautiani na mke wangu na wote wanaopendelea Kiingereza. Natamani kuona watoto  na wadogo zetu walio katika shule za sekondari na vyuo wakipata maarifa na ujuzi wa kutenda kazi mbalimbali. Ningependa kuona vijana hawa wanaohitimu wanaweza kutumia Kiingereza (na/au lugha nyingine za kimataifa) kuwapa urahisi watembeapo duniani kusoma, kufanya kazi au biashara.

Naamini kama wanavyoamini wengine kuwa Kiingereza kitawapa vijana faida na uwezo wa kushindana katika soko pana zaidi la ajira la Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na dunia.

Hata hivyo, kama tutazungumza ukweli, hali ya ufahamu Kiingereza wa wanafunzi kuanzia sekondari hadi chuo ni duni sana. Kadhalika, hali ya ufahamu wa lugha hiyo kwa sisi walimu wenyewe tunaotakiwa kuwafunza hao vijana pia ni wa shaka kubwa.

Nikiwa mwalimu wa chuo, nakiri kuwa si ajabu kukuta baadhi yetu, sisi walimu, tukipata tabu kuwasiliana kwa Kiingereza iwe darasani au penginepo, sembuse shule za sekondari

Kutokana na hali hii ya ufahamu wetu duni wa lugha, mara nyingi huwa najiuliza kwa kiasi gani uelewa wetu duni wa Kiingereza, lugha ambayo ndio njia ya kufikisha maudhui ya masomo husika, kutungia mtihani na kujibia inachangia katika matokeo mabaya ya mitihani ya kitaifa?

Wanasema pasipo kuwa na utafiti huna haki ya kuzungumza na mimi nisingependa kujibu swali hilo kwa kubuni, ingawa kuna ushahidi wa wazi, wa mazingira, unaoonyesha kuwa Kiingereza ni kikwazo.

Mwaka huu pekee watahiniwa 151,187 sawa na asilimia 42.91 wamepata sifuri katika matokeo ya mtihani wa mwaka jana yaliyotangazwa karibuni, kati yao wavulana ni 78,950 (asilimia 41.54) na wasichana ni 72,237 (asilimia 44.51), na hiyo ni licha licha ya kuanza kutumia mfumo mpya wa kupanga madaraja uliodhaniwa ungepandisha ufaulu.

Takwimu pia zinaonyesha kuwa watahiniwa waliopata daraja la nne ni 126,828 sawa na asilimia 36 , kati yao wavulana wakiwa 63,987 na wasichana wakiwa 62,841.

Hivi vijana hawa wote ina maana hawana akili kiasi hichoHatushtuki kwamba baada ya miaka minne ni vijana sita tu kati ya kumi ambao walau wameambulia kituHatushtuki kuwa katika kila wahitimu 10, wahitimu 7 wamepata kati ya daraja la sifuri na nne

Hivi hatushangilia kwamba baada ya miaka minne ya elimu ya sekondari ambayo mwanafunzi amekuwa akielimishwa fani mbalimbali kupitia Kiingereza, bado idadi kubwa ya wanafunzi tunaokutana nao mitaani hawawezi kuzungumza hata sentensi moja ya Kiingereza iliyonyookaKama mwanafunzi haelewi lugha ya kujifunzia ni wazi kuwa hata maudhui ya alichofundishwa anababaisha.

Kadhalika, tulifikiria nini tulipopanga Kiswahili kitumike shule za msingi halafu ghafla mwanafunzi akiingia kidato cha kwanza aanze kufundishwa kwa Kiingereza, huku fani zikiwa zimeongezeka na baadhi yazo ni mpya kabisa kwa vijana wetu. Mantiki ya mpango huu iko wapi?

Ni viashiria hivi ndivyo vinavyonifanya niamini kuwa umefika wakati sasa tutofautishe kati ya maudhui ya elimu na lugha ya kufikisha elimu hiyo kwa upande mwingine. Kadhalika, ni wakati muafaka sasa  tuchague kipi kati ya viwili hivyo tukipe kipaumbele.

Ninaposema tutenganishe viwili hivyo nina maana tusilazimishe kutumia maudhui ya elimu kusaidia wanafunzi kufahamu lugha tunayoitamani. Mtu aliyeelimika, ameilimika tu bila kujali alipata elimu hiyo kwa lugha gani. Pia mtu huyo anapaswa kuweza kutumia elimu hiyo kumsaidia katika maisha yake bila kujali alifundishwa kwa lugha gani.

Kwa sasa tunataka vyote kwa pamoja na matokeo yake tunababaisha katika maeneo yote mawili. Kiingereza hatukijui vizuri na maudhui ya elimu tunayofundisha pia tunababaishababaisha. Kisatumechanganya mambo mawili ambayo kimsingi ni tofauti.

Kimantiki, kwa kutumia Kiingereza, ambacho wengi hatukijui, ni kama tunasema nchi hii ili uelimika lazima ujue Kiingereza. Ina maana bila kujali mwanafunzi anakijua Kiingereza  au hukijui na walimu wanakijua au hawakijui – sisi tunakupa maarifa kwa lugha hiyo na kama huelewi imekula kwako

Mimi nilidhani kujua Kiingereza ni suala la hiari, lakini kuelimika ni suala la lazima. Tunachofanya ni kinyume cha hilo. Aina hii ya elimu ni kama tumeibuni katika msingi wa dhana kuwa tunawapa elimu watu wetu ili wakafanye kazi nchi zinazotumia Kiingereza, na si kwa ajili ya kuandaa wataalamu wetu.

Sasa jawabu la tatizo hili ni niniKama tunataka vijana wetu waelimike katika fani mbalimbali za sayansi, sayansi ya jamii, sanaa, biashara na uchumi inafaa tutumie Kiswahili kama lugha ya kufundishia kuanzia msingi hadi elimu ya juu.   Kiingereza ibaki kuwa lugha ya pili muhimu itakayowekewa mikakati maalumu ya kuboresha ufundishaji wake.

Mkakati  muhimu wa kwanza ni kuweka Kiingereza kama somo la lazima katika ngazi zote za elimu kuanzia chekechea hadi shahada ya kwanza. Pili, tuwe na mpango wa kuimarisha mafunzo ya Kiingereza, hususan, kwa kuboresha mafunzo kwa walimu. Pia, katika mafunzo ya Kiingereza msisitizo uwekwe katika kuwawezesha vijana si tu kuandika, bali kuzungumza Kiingereza kwa kujiamini.

Nasisitiza mafunzo ya kuzungumza kwa kujiamini kwa sababu Kiingereza chetu “kilichovunjika vunjika” kimetusababishia maradhi mengine ya kutojiamini katika majukwaa ya kimataifa maana tumejiaminisha kuwa kuzungumza Kiingereza kibovu ni jambo la aibu.

Nimesoma shahada ya kwanza Uganda, huko tulikuwa Watanzania wengi katika darasa langu. Utatujua Watanzania kutokana na ukimya wetu maana tunaogopa kuchekwa na kigugumizi cha kutafuta maneno.

Hapa China, nimekutana na wachina wengi ambao wana Kiingereza kichache na cha kubabaisha lakini wanakizungumza kwa kujiamini. Nchi za Asia: Korea, China na Japan wanatumia lugha zao kufundishia huku wakifundisha vijana Kiingereza  kama somo ili kuwasaidia wanapohitimu kutumia fursa zinazojitokeza duniani kote za elimu au ajira.

Wapo watakaokosoa mawazo yangu kwa kuhoji kwa nini tusiimarishe mafunzo ya Kiingereza na kuendelea kukitumia kama lugha ya kufundishiaHiyo ina maana tuwapige msasa walimu wa masomo yote ili wakimudu Kiingereza na kufanya hivyo kunahitajika rasilimali na muda mrefu zaidi, wakati uharibifu unaendelea.

Watanzania tuna bahati kwani tunayo lugha moja inayotuunganisha, Kiswahili, tofauti na nchi nyingine nyingi za Kiafrika. Kwa nini tusitanue matumizi yake na kuifanya lugha hii kuwa ya kufundishia, walau mpaka shahada ya kwanza

Najua wapo watakaonituhumu kuwa huenda natokea katika daraja la watu wenye uwezo wa kulipia watoto ada  katika shule bora za binafsi ambako wanafunzwa kwa Kiingereza na kwamba siwatakii mema Watanzania walio wengi ambao labda hawana uwezo wa kulipia shule binafsi.

Kwanza,  yangu ni sauti ya mlalahoi anayehangaika kama wengine kuhakikisha watoto wao wanapata elimu nzuri, lakini hebu tuichunguze hoja hiyo kama ina mantiki.

Kwa mfumo uliopo wa Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia kuanzia kidato cha kwanza hadi cha taasisi za elimu ya juu, nani anafaidika na nani anaathirika. Wanaofaidika ni wale wale walio na fedha za kulipia watoto wao ada katika shule binafsi zilizo bora na tunaoathirika ni sisi walalahoi tunaopeleka watoto wetu shule za serikali na za binafasi za daraja la chini.

Sisi tunaoathirika katika mfumo huu tunapata madhara mara mbili. Kwanza vijana wanahitimu bila elimu (hawana ujuzi, maarifa na utambuzi finyu wa mambo). Kadhalika, hicho Kiingereza kinachosemekana kuwa kinatumika kuwafundishia pia hawakijui.

Tukitumia Kiswahili, kuna uwezekano mkubwa wa wanafunzi kuelewa maudhui ya elimu, na watakuwa pia na fursa ya kujifunza Kiingereza, ambacho naamini anayetaka kukifahamu akiweka jitihada atafanikiwa.

Hoja ya Kiswahili kukosa misamiati ni butu kabisa. Lugha zinakopa maneno ya kitaalamu. Na sitaki kuamini kuwa mwalimu aliyeelewa dhana fulani atashindwa kuielezea kwa Kiswahili akaeleweka. Kama anashindwa, basi yeye mwenyewe hakuielewa.

Kadhalika, maandalizi yatapaswa kufanyika kabla ya utekelezaji wa uamuzi huu kwa  kuziwezesha taasisi zetu za kuendeleza Kiswahili kuandaa istilahi za masomo mbalimbali kwa kushirikiana na wataalamu wa masomo husika ili kupata visawe vinavyoeleweka kulingana na misingi ya Kiswahili. Pia,  wataalamu hawa wanaweza kutayarisha makala na vitini vya kufundishia.

Kwa hali ilivyo sasa, ninapoona hali ya matokeo ya Wilaya yangu ya Tunduru, ambako zaidi ya asilimia 70 ya wanafunzi wamepata sifuri, pamoja na matatizo lukuki mengine, sitaacha kulaumu matumizi ya Kiingereza maana huwa nakutana na wanafunzi waliomaliza kidato cha nne, na, huwa sielewi inakuwaje mwanangu wa miaka minne aliye chekechea anazungumza Kiingereza kuliko wao

Njonjo Mfaume

 

njonjo.kweja@gmail.com

Njonjo Mfaume ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Shule ya Habari na Mawasiliano ya Umma. Kwa sasa yuko masomoni nchini China.

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s