VITAMBULISHO na HOJA ya UGHAIBUNI

fredy_machaVITAMBULISHO TANZANIA na HOJA ya UGHAIBUNI

Na Freddy Macha,Mwananchi

KWA UFUPI

Sisi hohehahe, lakini tunapoambiwa vitambulisho vitazuia uhalifu, tayari tunafikiria kero tu ya Serikali. Nakumbuka mwaka 1981 nilisimamishwa usiku mmoja, mjini Dar es Salaam.

Hivi karibuni baadhi ya wananchi wamelalamikia suala jipya la vitambulisho. Wanadai linakera; eti watu wameuawa. Kuna upendeleo, ugumu na mambo kama hayo.

Kabla ya kusafiri kwenda ughaibuni miaka 30 iliyopita, wakati wanamgambo walipokuwa wakisimamisha wazalendo barabarani na mitaani kudai vitambulisho, mimi vilevile nililiona suala hilo ni unyanyasaji wa Serikali.

Baada ya kutembea na kuishi nchi nyingi duniani, nimegundua vitambulisho ni jambo la kawaida. Tofauti ipo katika namna vinavyoulizwa au vipi sera hiyo inavyotekelezwa na vyombo husika.

Tunavyojua, suala la vitambulisho liliasisiwa Tanzania mwaka 1968 kwa sababu za kiusalama baina ya nchi jirani na marafiki Afrika Mashariki na Kati.

Baada ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjika (kutokana na sababu mbalimbali, mojawapo kufariki Rais Jomo Kenyatta wa Kenya, mwaka 1978 na Serikali dhalili ya Jemadari Idi Amin wa Uganda iliyoangushwa 1979), sera hiyo ilifuata.

Hadi leo suala hilo limekuwa likifufuka na kutoweka, bila kujikita na kukaa kitako muda mrefu kama ilivyo mataifa mengine. Ndiyo maana leo ni jambo geni na kero kwa raia, hasa vijana.

Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa Tanzania (NIDA), imeorodhesha vipengele kumi na moja vinavyoelezea faida kuu za vitambulisho. Katika orodha hiyo kipengele cha saba kinaeleza; “Vitambulisho vitafanikisha kuhakikisha mtu anapata stahili zake za jamii. Kwa mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za pensheni, haki za matibabu, haki za kujiunga na masomo ikiwa pamoja na stahili zozote ambazo raia Tanzania anastahili.”

Kimtazamo ni ahadi nzuri na muhimu. Naomba nichangie namna mambo yanavyokuwa huku Ughaibuni.

Kwanza, kila mwananchi hufahamika amezaliwa lini, wapi, anaishi na kufanya kazi gani na kadhalika. Unapohitaji huduma yoyote, lazima uwe na anuani kamili ya unapoishi. Kama huna huipati. Huwezi kuishi kiholela bila anuani.

Mawasiliano au barua zozote huletwa nyumbani kwako. Kinyume na kwetu Tanzania, ambako hakuna mpangilio kamili wa anuani za kila mtu, nchi zilizoendelea huorodhesha anuani zote; hakuna kujificha.

Kwetu tunapoandikiwa barua hubidi kwenda posta kufungua kasha, au kazini ulikoajiriwa. Serikali ya Tanzania ina kazi kubwa kujua kila raia alipo. Matokeo yake maskini wengi wasiojulikana na Serikali, huishi tu bora twende, wakitegemea kudra ya Mwenyezi Mungu na bahati nasibu.

Huku Uzunguni suala la kujulikana unakoishi, huendana na suala la ‘kutawaliwa na kulindwa’ vilevile. Tatizo linapotokea, mathalan, ajali ndani, au hata uzoaji takataka (wa kila juma )- huwa rahisi kufakinikishwa na vyombo husika. Utamaduni huu unaendana na hulka ya uhuru na demokrasia. Je, sisi tunayo?

Kipengele cha tano cha faida iliyoahidiwa na NIDA ni uhalifu na usalama. Ulimwengu leo umekithiri ugaidi na ujambazi hasa wa dawa za kulevya. Afrika imeshageuzwa ‘uwanja wa fujo’ wa magaidi wanaotumia dini na ujambazi wa dawa za kulevya.

Ni rahisi kuzuia uhalifu ikiwa kila habari za mwananchi zipo ndani ya mfumo wa ulinzi (data base).

Sisi hohehahe, lakini tunapoambiwa vitambulisho vitazuia uhalifu, tayari tunafikiria kero tu ya Serikali. Nakumbuka mwaka 1981 nilisimamishwa usiku mmoja, mjini Dar es Salaam. Hali ilikuwa mbaya. Bidhaa muhimu hazikupatikana; walanguzi walikwenda nchi jirani kusaka vitu (hasa mitumba) vilivyouzwa bei za juu na kupewa jina; mwendo wa kuruka.

Jioni hiyo nilifuatana na kijana mwenzangu na dada wawili, mitaa ya Kinondoni tulipopitia baa kadhaa. Kufika Mwananyamala, mgambo walitusimamisha kwa jazba. Mosi ilikuwa wale dada wazuri wazuri. Pili, tulishauchapa mtindi; tumechangamka. Tatu, tumebeba vifurushi. Mimi nilikuwa na shati nililonunua kutoka kwa mpigania Uhuru wa Afrika Kusini. Shati zuri la rangi rangi ambalo halikupatikana Bongo.

“Ndugu, simameni!” (Enzi hizo maneno “bwana au waheshimiwa” hayakutumika).

“Wapi mnakwenda, wapi mmetoka?”

Tukasema tumetoka kazini, tukapitia baa; tunaelekea nyumbani.

“Mmebeba nini, ndugu?”

Tukaonyesha mitumba.

“Hizi siyo nguo za Mzee Kambarage” (alivyoitwa Mwalimu). Mimi nikasema ni mwanahabari, pia ninafanya kazi na wageni, nimepewa zawadi kazini. Ukweli niliajiriwa kama mkalimani Ubalozi wa Misri. “Wapi kitambulisho chako?”

Bahati mbaya siku hiyo sikukibeba. Hakikuwa tayari. Vilitakiwa kubadilishwa nembo baada ya mauaji ya Rais Anwar Sadat. Wamisri walikuwa na Rais mpya wa muda, Hosni Mubarak. Ikawa kasheshe. Malumbano, simu za mkononi miaka hiyo ilikuwa njozi tu za malaika. Huwezi kumweleza mgambo subiri nimpigie bosi simu adhihirishe unalolidai.

“Hizi nguo za magendo ndugu. Siyo za Kitanzania. Itabidi mziache hapa hapa.”

Baada ya maneno mengi, yakaisha. Maneno hayo yalimalizika kwetu kuwapa wale jamaa ‘chochote’…Msomaji, zingatia hilo.

Hiyo ndiyo dunia ya vitambulisho miaka thelathini iliyopita, Tanzania.

Sasa, nikupelekeni Brazil, miaka kumi baadaye. Nimetoka kazini usiku (kupiga dansi) mjini Rio De Janeiro. Nimempa lifti mmoja wa wacheza dansi wa bendi. Aliishi Mtaa wa Tijuca, kaskazini ya jiji, ni mbali. Wakati nikirejea, nikasimamisha gari kutimiza haja ndogo; ghafla nikazingirwa na taa kali za magari. Bunduki, kelele, vitisho. Yote kwa Kireno.

“Piga magoti, mikono juu.”

Askari wengine wameingia kwenye gari wanalipekua. Kwa vile nilikuwa na nywele ndefu za Rasta, wale askari waliokuwa wakipiga tarumbeta wakaniita palepale “jambazi” muuza dawa za kulevya. Nikakataa katakata; mikono juu. Kwa Marekani Kusini, ni kawaida wananchi kuuawa na askari, popote pale hasa usiku hadi leo. Nikasema mimi mwanamuziki, wathibitishe kwa gitaa langu ndani ya gari.

“Ah wapi, tunakujua wee muuza bangi mkubwa.” Mimi ni mwanamuziki; nikajitetea.

“Wapi kitambulisho?”

Nikasema kiko mfukoni. Naweza kushusha mikono nikitoe? Hawakuniamini. Wakidhani nitatoa bastola. Mmoja akanisogelea akachomoa pochi. Kakuta pesa na kitambulisho. Huendi kokote Brazil bila kitambulisho.

Lakini kilikuwa kitambulisho maalumu cha wageni( “Estrangeiro”). Anuani ya kitambulisho ilionyesha hakika, naishi mtaa wa wageni.

Sasa wanataka “kunitoa upepo.” Haraka nikasema jirani na rafiki yangu ni afande wao mkuu kanali (fulani). Waliposikia jina, wakagutuka. Tena sana.

Nikawaomba wampigie simu wamuulize. Simu ikapigwa. Kanali akasema kweli ananifahamu; isitoshe anaipenda sana bendi yetu inayopiga klabu maarufu ya Columbus ufukweni mwa, Copacabana, Rio De Janeiro.

Unaona visa hivi viwili vilikoanza na vilikoishia? Kwa wale mgambo Mwananyamala bila ‘malipo’ ingekuwaje? Je, hawa wenye mitutu ya Ibilisi? Nisingefahamiana na huyo kanali mkuu ningekuwa hai leo kweli?

 3

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s