SERIKALI ITOE ULINZI

SERIKALI ITOE ULINZI kwa VIPAJI na UBUNIFU vya WATANZANIA                      Na Assumpta Nalitolela

KWA UFUPI

Mimi naiomba Serikali isiwafikishe wasanii huko; iwajibike na itengeneze mikakati ya kulinda kazi za wasanii sasa kwa kuhakikisha haziibwi. Zikiibwa basi hatua kali zichukuliwe dhidi ya wezi husika.

Yapo mambo ambayo mtu anawajibika kuyafanya mwenyewe, pia yapo ambayo Serikali inapaswa iyafanye kwa watu wake.

Mtu anawajibika kufanya kazi kwa bidii ili atengeneze kipato kwa ajili ya ustawi wa maisha yake na familia yake.

Kwa kipato hicho atapanga au kujenga nyumba, atazalisha au kununua chakula kwa ajili yake na familia yake.

Mambo haya yatatekelezwa na mtu, itakuwa kichekesho kikubwa kama mtu atakwenda serikalini na kuomba chakula, mavazi na malazi katika hali ya kawaida.

Inawezekana kama kulikuwa na maafa kama mafuriko, ukame na mengineyo, ambavyo viliathiri upatikanaji wa mambo hayo. Hapo Serikali itasaidia, lakini katika hali ya kawaida jukumu hilo nl la kila Mtanzania mwenye uwezo wa kufanya kazi.

Serikali nayo kwa upande wake ina wajibu wa kulinda vile ambavyo raia wanavitolea jasho kwa ajili ya ustawi wa maisha yao. Kuwepo na ulinzi katika mali aliyoichuma, kazi alizozitengeneza na haki zingine licha ya ulinzi wa uhai wake mwenyewe.

Raia wana mchango katika usalama wao na mali zao, lakini zaidi ni ule wa kutoa ushirikiano kwa vyombo vinavyohusika kwa njia ya kutoishi katika mazingira hatarishi, kutoa taarifa pale usalama unapotoweka, kusaidia kumkamata mtu anayehatarisha usalama wa raia na mali zao na kumpeleka mahali panapostahili.

Tunaziona juhudi za Serikali katika kulinda mali za raia wake kwani kila siku tunaona angalau mikakati ya kupambana na wezi, majambazi hata majangili pamoja na kasoro za hapa na pale.

Kitu kimoja ambacho Serikali imekisahau ni ulinzi wa taaluma, vipaji na ubunifu wa raia wake. Vipaji na ubunifu wa wenye navyo unaibwa, huku wanaoibiwa wasijue cha kufanya. Hakika katika hili Serikali tuinyoshee vidole.

Serikali imeshindwa kulinda ubunifu na vipaji vyetu. Wasanii wamelia miaka mingi kazi zao kunakiliwa bila vibali vyao na kuwafanya watu ambao wala hawakutoa jasho katika kuitengeneza kazi ile kuneemeka zaidi kuliko wasanii wenyewe.

Zipo taasisi zilizoundwa kulinda hati miliki za kazi hizo za vipaji na ubunifu kama COSOTA, lakini nikionacho mimi ni taasisi hiyo kujihusisha na ukusanyaji wa ada za kazi zaidi, kuliko kuzilinda kazi hizo.

Sijawahi kusikia juhudi zozote zilizofanywa na COSOTA kulinda kazi ya msanii. Wizi wa kazi za wasanii ni janga ambalo siyo rahisi kwao kujilinda mwenyewe.

Kama ataruhusiwa kufanya hivyo, basi yatakayotokea asiambiwe tena amejichukulia sheria mkononi mwake mwenyewe.

Kazi ya ulinzi huo ni ya Serikali. Mimi siwezi kutoa ushauri ifanye nini lakini, hatua zilezile inazochukua kuwalinda wakulima dhidi ya vipimo kama vya lumbesa, ambapo mkulima hupunjwa bei ya mazao yake kwa kuongezewa ukubwa wa gunia analouzia mazao.

Ni juhudi hiyohiyo tunaihitaji katika kulinda kazi za wasanii. Serikali ije na mikakati ya namna gani kazi za wasanii zitalindwa; ibebe jukumu hilo na kumwona mwizi wa kazi za wasanii kama mwizi mwingine yeyote na hatua kali zichukuliwe dhidi ya wezi hao.

Kama watachukuliwa kimzaha, kama vile tunavyoona sasa iko siku tutasikia wasanii wamejichukulia sheria mikononi mwao; nao wakawachoma wezi wao, wakaunguza maduka yanayouza kazi zao zilizonakiliwa.

Mimi naiomba Serikali isiwafikishe wasanii huko; iwajibike na itengeneze mikakati ya kulinda kazi za wasanii sasa kwa kuhakikisha haziibwi. Zikiibwa basi hatua kali zichukuliwe dhidi ya wezi husika.

Naamini kwa mkono mrefu ambao Serikali inao ikitaka italinda kazi hizo. Kazi za wasanii zikilindwa ndivyo Serikali itakavyoweza kuongeza mapato yake kupitia kodi zitakazotolewa na kazi hizo za wasanii.

Serikali itambue pia kwamba kuna wizi mkubwa wa vipaji na ubunifu wa wafanyakazi sehemu mbalimbali za nchi hii kwenye kampuni za kigeni hata za Watanzania wenyewe.

Ni ukweli kabisa tuko kwenye soko huria, likiwemo soko la ajira, lakini soko hilo huria linapaswa kudhibitiwa la sivyo Watanzania watalishwa visivyostahili kuliwa.

Inaumiza kuona kwamba vipaji na ubunifu wa Watanzania sehemu nyingi za kazi havilipiwa ujira unaotakiwa. Nimewahi kuhoji hata katika moja ya makala zangu kwamba inakuwaje mtu anaajiriwa halafu nusu ya mshahara wake unakwenda kwa taasisi iliyomtafutia kazi, tena siyo kwa mwezi mmoja bali kwa miezi yote atakayokuwa kwenye ajira hiyo.

Kama hajaajiriwa kupitia taasisi hizo za ajira basi anaweza akajiunga na kazi na asilipwe mshahara bali apewe posho kidogo kwa mwaka mzima. Huu ni wizi wa taaluma za Watanzania.

Tusisema “kwani mtu kalazimishwa kwenda kufanya kazi kwa wezi hao?” Jamani hali ya ajira sote tunaijua, mtu kazunguka na vyeti vyake mpaka soli ya kiatu ikaisha, halafu anakutana na fursa hiyo ya kazi ataiachia wakati hana kitu mfukoni? Hata ungekuwa wewe msomaji wangu ungeikubali kazi hiyo angalau kwa muda mfupi, wakati unaendelea kutafuta nyingine.

Kwa kuwa hakuna adhabu kwa atakayeshindwa kumlipa mtu kiwango cha chini cha mshahara kwa sekta husika, basi mwajiri anaamua kumlipa mtu Sh50,000 kwa mwezi, mtu anayemfanyia kazi za kuingiza mamilioni.

Yeye ananeemeka, wakati wafanyakazi wake wanajaza madeni, magonjwa ya moyo na kukata tamaa ya kuishi.

Waajiri wa sekta binafsi wanaitumia vizuri fursa hii ya kukosekana kwa kazi kwa wahitimu wa vyuo. Wanajua kwamba soko limefurika hivyo wanaweza kucheza na maisha ya watu kadiri watakavyo.

Akiacha kazi huyu kwa kutoridhika na masilahi. atakuja mwingine, hivyo kwa nini mwajiri atoe pesa yake kwa kulipa vizuri wakati anaweza kuwapata wafanyakazi kwa bei sawa na bure.

Hapa ndipo Serikali inapotakiwa kuingilia kati kulinda raia wake, wasijisikie kama wanafanya kazi nje ya nchi yao.

Naishauri Serikali iwe na kitengo kitakachoratibu na kufuatilia mienendo ya waajiri katika sekta binafsi, bila hivyo Watanzania wataendelea kuibiwa kwa mtindo huu na kuishia kukata tamaa katika nchi yao wenyewe kana kwamba hawana serikali ya kuwalinda. Serikali inaweza kufanya hivyo.

Jumapili njema

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s