SAUTI za WASANII kwa BUNGE la KATIBA

Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Posted  Marchi 29  2014  saa 15:32 PM

KWA UFUPI

  • Hivi sasa Tanzania ipo katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya, hii ni nafasi ya kipekee kabisa ya kutengeneza taifa jipya. Katiba hii ndiyo ngao itakayowalinda Watanzania kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.

Inahitajika sheria ili kufanya biashara ya sanaa nchini. Kwa kipindi kirefu sasa wasanii wamekuwa wakipiga vita wizi kazi za sanaa, pamoja na urasimishwaji.

Hivi sasa Tanzania ipo katika mchakato wa kuandaa Katiba Mpya, hii ni nafasi ya kipekee kabisa ya kutengeneza taifa jipya. Katiba hii ndiyo ngao itakayowalinda Watanzania kwa zaidi ya miaka 50 ijayo.

Rasimu ya Katiba iliyoanza kupitiwa na wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba imetajwa makundi mengi sana lakini imeacha wasanii ambao ni sehemu kubwa ya jamii, wao wanachukua robo ya Watanzania wote.

Wasanii wameamua kupaza sauti zao na kudai haki ambayo wameshindwa kuipata katika kipindi cha katiba ya mwanzo, huku wakisaidiwa na baadhi ya wanasiasa ili kuhakikisha mapendekezo yao kuhusu Katiba Mpya waliyowasilisha kwa Tume yanafanyiwa kazi.

Ombi kuu la wasanii ni kuhakikisha kazi ya sanaa inathaminiwa kama kazi, huku wakihitaji kazi zao, miliki bunifu kuthaminiwa na kulindwa.

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba anasema kuna kila haja ya kurasimisha sanaa na kuitambua kama sekta rasmi.

“Maisha ya taifa na urithi wa taifa unahifadhiwa katika kazi za sanaa, iwe ni katika nyimbo, mashairi, michoro, riwaya au maigizo na kazi nyinginezo, kazi zinazotokana na vipaji na bidii za Watanzania. Taifa lisilotambua na kuthamini kazi za sanaa ni taifa lisilojitambua, tuanze kujitambua kwa kuwatambua wasanii na kuzilinda kazi zao kwenye Katiba hii mpya,” anasema January Makamba.

Mbali na mwanasiasa huyu, wabunge wengine Livingstone Lusinde (Mtera mkoani Dodoma) na Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), maarufu Sugu, pia wameungana na wasanii hawa katika kampeni hii muhimu.

Wasemavyo wasanii

Umoja wa wasanii wote nchini kupitia shirikisho la sanaa, unataka sanaa irasimishwe kwa maendeleo ya sasa na yajayo, IP (intellectual property right) miliki bunifu  kwenye sanaa kwani ndiyo ngao yao, na isipowezekana leo haitawezekana mpaka miaka 50 ijayo.

Wasanii wengi wa rap na hiphop wanasema kuna haja ya Serikali kuangalia upya, kwani Tanzania ina zaidi ya wasanii milioni 10, lakini kilio chao kikubwa  wameachwa na hawatambuliki katika Rasimu ya Katiba inayopitiwa bungeni Dodoma.

Mchizi Mox yeye anasema kutokuwekwa sheria ya kuitambua sanaa kama sekta rasmi ni kuukandamiza uchumi wa nchi.

“Makundi mengi yametajwa ila wameacha wasanii, kwa nini wakati ni kundi kubwa katika jamii tupo zaidi ya milioni 10, na tunachangia uchumi wakitutosa wasanii ni kama wameukandamiza uchumi,” anasema.

P Funk naye ni mmoja kati ya wasanii wa hiphop aliyeamua kuingia katika kampeni hii, “Bila Serikali kututambua kwenye Katiba Mpya, sanaa haiwezi kusonga, itakuwaje nina kipaji lakini niishie kupiga miayo, huu ni mchakato wa miaka 50 ijayo lazima tuwe makini.”

Kala Jeremiah yeye anasema, “Tunafundisha, tunaelimisha mila na desturi kiutamaduni, tunaburudisha jamii, tutambulike kikatiba siyo tutambulike baa tununuliwe bia mbili wakati nyumbani kuna njaa.”

Kauli ya mwanahiphop huyo inaungwa mkono na Dani Misimamo ambaye anasema “Wino kwenye kalamu mpaka kwenye rasimu, unaposema hii ni ajira isiyo rasmi huo ni utaahira ulio rasmi hiki ni kilio cha hasira kutoka kwa wasanii.”

Wakati huohuo, Fid Q anasisitiza sanaa isiwe ngazi ya kutengeneza maskini wenye majina makubwa. “Sanaa ya muziki, filamu maonyesho na ufundi ni kazi iko wazi kikatiba tutambulike ili tuweze kuwa na majina makubwa yanayolingana na hadhi yetu ya umaarufu,” anasema.

Wasanii bado wanalalamika kutokana na Serikali kuamua kurasimisha sanaa na wasanii kuanza kulipa kodi, lakini bado hawajaweza kuwaingiza katika Rasimu ya Katiba.

“Kodi zetu wanachukua kivipi hawatutambui, kodi zetu wanachakachua uchumi wetu haukui tuheshimike kikatiba, sanaa ni ajira kamili, saa ya ukombozi ni sasa katiba ilinde hili,” anasema Profesa Jay.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mwana FA; “Mabilioni yanapotea wameamua kuyafumbia macho, mnatutia ufukara sisi na vizazi vijavyo, kama sanaa inalipa kwanini isirasimishwe au mmeamua uharamia uhalalishwe, katiba itutambue wasanii, sanaa ni ajira ya kudumu hii, ni chanzo kikubwa cha uchumi viwepo vifungu kulinda tunavyobuni.”

Kalapina naye anasema; “Sanaa ndiyo maisha yetu, tunaishi, tunakula sisi na watoto wetu, tupo wengi sana zaidi ya wavuvi na wafugaji, sanaa ni kazi pia vipaji.”

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s