AFYA YA VIJANA WA LEO NI MBAYA UKILINGANISHA NA ENZI ZETU

fredy_machaNa Freddy Macha

Posted  Jumapili,Aprili 20  2014  saa 14:45 PM

KWA UFUPI

Nikamshauri awatazame wengine pale. Kila mmoja alikuwa akifuata utaratibu maalum. Baadhi walibeba vijitabu au vijikaratasi vilivyoandikwa mpangilio wa mazoezi.

Wiki iliyopita mwanasoka maarufu, Yaya Toure, alikumbusha suala la afya alipofanya mahojiano na gazeti mashuhuri Uingereza- Daily Mail.

Yaya anayeichezea Manchester City ni kati ya Waafrika kutoka Ivory Coast pamoja na kaka yake Kolo Toure na Didier Drogba waliojenga majina Ulaya.  Aliyekuwa akimhoji, Jammie Rednapp ambaye ni mchezaji wa zamani Liverpool alitaka kujua je mpira Ulaya ni tofauti na Afrika?  Yaya Toure, ambaye ni mrefu na pandikizi la mtu akajibu haraka:  “Nilichezea kwanza Metalurh Donetsk na ilikuwa tofauti sana. Ndiyo nimehama Afrika; nikaanza kujifunza namna ya kula sawa sawa, kupumzika, kuweka fikra zilizotulia na kuelewa michezo katika ngazi za juu.”

Tuangalie nahau:  “Nikaanza kujifunza kula sawasawa…”

Nilipofanya warsha mjini Dar es Salaam mwaka 2009 na 2011 nilikutana na vijana Watanzania kadhaa wanasoka. Wapo waliolalamika kichomi na kukaza musuli. Musuli (hasa ya miguu na mikono) inapokataa kunyooka na kulegea sawa sawa (“cramp”), ama unapocheza au ukiwa tu umekaa, kuna tatizo la mzunguko wa damu. Tatizo hili hutokea kama tuna kula vyakula vyenye chumvi nyingi.  Chumvi ikizidi huathiri mishipa ya damu, moyo. Hizi ni baadhi ya nguzo muhimu za ulaji kwa wanamichezo na hata sisi wengine.

Miezi michache iliyopita tulikuwa Gym na kijana mmoja wa Kitanzania aliyewasili Ulaya karibuni. Kuingia tu pale bwana mdogo aliparamia kila kifaa. Mara kile, mara hiki. Hakuwa na mpango maalum.  Nikamuuliza: “Je, ndivyo huwa unafanya mazoezi?”  Akasema ndiyo.

Nikamshauri awatazame wengine pale. Kila mmoja alikuwa akifuata utaratibu maalum. Baadhi walibeba vijitabu au vijikaratasi vilivyoandikwa mpangilio wa mazoezi.

Wapo waliotumia simu zao kufuata wakati. Chuma hiki kitakuwa dakika fulani, kile dakika fulani. Kifupi uinuaji vyuma si wa hobela hobela. Unatakiwa ujiulize…

Je, unatafuta nguvu, musuli, ukubwa wa mwili, au unapunguza unene?  Mazoezi unayafanya muda gani? Mathalan, siku hizi kwa kuwa Watanzania wengi tumegundua kufanya mazoezi ni muhimu (kupunguza unene) utamkuta mtu anakimbia au anafanya mazoezi kila siku ya Mungu.

Haiendi hivyo. Lazima uwe na nidhamu na utaratibu. Mwili unatakiwa kupumzika. Kama alivyosema mwana kandanda, Yaya Toure. Kupumzika ni muhimu kama yalivyo mazoezi yenyewe. Ikiwa leo utafanya mazoezi makali yatakiwa kesho upumzike kabisa.

Wakati wa mapumziko watakiwa sasa uangalie mlo. Mada ya kula nayo ni dhahabu.

Kuna jamaa fulani nilifanya naye mazoezi, lakini hanywi maji wakati wa mazoezi.  “Nakunywa glasi zangu tatu, nne kwa mpigo basi. Asubuhi. Zinan’tosha siku nzima.”

Hapo ndipo wananchi tunakosea.

Unywaji maji watakiwa uwe wa kadiri (glasi au bilauri au kikombe kwa mpigo) mara kwa mara, siku nzima. Kama ilivyo chakula si kunywa maji mengi, halafu, basi.

Wengi tumezoea kunywa maji, pombe au chai wakati wa kula. Wataalamu wanashauri kutofanya hivyo kwa sababu mbili. Mosi, umeng’enywaji wa chakula (“digestion”).

Chakula kinapoliwa huanza kumeng’enywa mdomoni kwa mate.  Unapokitafuna haraka haraka (kubugia) na kumezea na kinywaji unapunguza nguvu zake. Ndiyo matokeo, mtu anacheua ovyo, na hata asipocheua kuna hatari za tumbo kujaa haraka, kuvimbiwa.

Pili, kwa kuwa umeng’eywaji wa vyakula mbalimbali na vinywaji ni tofauti (kutokana na shughuli na kazi mbalimbali za tumbo) ni vyema kutenganisha. Ni kama kuchanganya mchanga, samadi, udongo na saruji kujenga nyumba. Kila kimoja kina nafasi yake.

Ni muhimu kunywa maji kidogo kabla ya mazoezi, kuendelea kuonja kidogo kidogo wakati unayafanya na mengi unapomaliza.  Jambo lingine ni urefu wa mazoezi. Wataalamu wa michezo na afya wanasisitiza kiasi cha dakika 45 hadi saa nzima tu, yatosha kwa mazoezi mara mbili tatu, kwa juma.  Unapozidisha, ukafanya zaidi ya saa mbili, au kila siku mfulululizo bila kupumzika, unaudhalilisha tu mwili.  Yaya Toure alitaja ulaji. Je, unakulaje baada ya mazoezi?

Wengi bado hatuelewi umuhimu wa uwiano kati ya vyakula vikuu vitano : wanga ( wali, ugali, na vingine), protini (nyama na mboga za majani), vitamini (matunda, mboga), madini (mboga za majani, korosho, karanga mbichi,) na mafuta asilia (maparachichi, nazi, maziwa mgando).

Ulaji wa wanga na protini (nyama) zaidi bila mboga za majani mabichi (saladi : matango, nyanya,) ndiyo moja ya tatizo kubwa letu Waafrika. Jambo hilo linawaathiri pia wanamichezo wetu na hususan vijana wanaojaribu kuinua vyuma au wafanyakazi sulubu na maofisini.

Wengi leo hatupiki tena vyakula asilia. Tunaparamia viazi vya kukaanga (“chips”) na nyama bila mboga za majani, matunda. Matokeo ya ulaji huu usio na mpango, ni kutaabisha miili rijali ya vijana.  Tunaposumbuliwa na vichomi, kuchoka ovyo au mistuko ya moyo ni dalili za dosari. Kitakwimu, wachezaji mpira wengi wanakufa kwa mshtuko wa moyo wakiwa uwanjani karibuni kuliko miaka thelathini au hamsini iliyopita.

Kwa nini? Matatizo yanakwenda sanjari na hali halisi. Leo kuna ushindani mkubwa, harakati za umaarufu, kupatikana habari haraka kupitia runinga, mitandao na simu. Kijana ana mengi ya kutamani kuliko miaka arobaini iliyopita.

Kwetu Tanzania sasa. Siku sisi tunakua, siasa ya Ujamaa ilikataza ubepari, ubwanyenye. Majarida, video au magazeti ya ngono yalikatazwa na hayakuonekana kabisa Tanzania. Mimi niliona sinema ya ngono (dhahiri) mara ya kwanza baada ya kusafiri nje nikiwa tayari mtu mzima.  Leo vimejazana. Matokeo vijana wanakosea wanapodhani “ngono” ni mapenzi; ilhali, ngono ni matokeo ya mapenzi na mahusiano mazuri.

Wiki iliyopita Serikali ya Uingereza ilikuwa ikitathmini, kutafakari na kudadavua urahisi wa watoto wa Kiingereza kutazama ngono. Urahisi huu umewafanya vijana wa kiume wawaone wasichana ni vyombo tu.  Kunavunja maadili na heshima kiasi ambacho kesi za watoto wadogo wa kiume wenye miaka 12 kuwabaka wasichana wadogo wa miaka minane au kumi zimeenea Uzunguni.

Kwetu Tanzania mitandao na mabloga maarufu kama “Mwanamke na Nyumba” huzungumzia namna wanawake wanavyolalamika wanaume leo hawajui kufanya mapenzi, na kama wanafanya hawana nguvu za kiume.  Hizi ni dalili za matatizo makubwa.  Elimu na maarifa ya kiafya si nzuri; vijana wanakua haraka, hawaelekezwi na matokeo hawafanyi shughuli sawasawa. Moja ya matokeo ya kutokula au kutofanya mazoezi sawasawa ni kupoteza nguvu za urijali.

Tuendelee na mada juma lijalo.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s