MUZIKI wa AFRIKA ni KIBOKO DUNIANI

fredy_macha

Saturday, 22 January 2011 20:59
Na Freddy Macha
MAFURIKO ya maji  Australia na  Brazil yameua wengi.  Karibuni nilimhoji Dave Marama mwanamuziki mkongwe aliyeshapiga na bendi mbalimbali nchini.  Mpiga gitaa huyu stadi aliondoka Dar es Salaam mwaka 1991 kwenda kuishi Australia na familia yake.  Miezi michache iliyopita bendi yake, Public Opinion Afro Orchestra, iliheshimiwa taji la ARIAS ambalo ni kama Grammy ya Wamarekani.  Heshima hii ya hali ya juu imetokana na CD inayoendeleza muziki wa Afro Beat uliobuniwa na Mnigeria Fela Kuti aliyefariki 1997.Dave Marama aliwahi kurekodi, kupiga au kukutana na magwiji wakubwa wa muziki Afrika mathalan, Hugh Masekela(Afrika Kusini), Oliver Mtukudzi (Zimbabwe), Femi Kuti (mwanae Fela), Baaba Mal (Senegal) na mzee wa Sax, Manu Di Bango (Cameroon).  Hivi karibuni nilikutana naye na kuzungumza naye kama ifautavyo:

Swali: Mafuriko si mchezo
Jibu: Hali mbaya hasa jimbo la Queensland na New South Wales.  Leo mto umetulizana kidogo lakini uokozi na matengenezo bado yanaendelea.
Swali: Australia pazuri?
Jibu: Nimeshapazoea.  Tuna Jamii ya Watanzania Australia  hivyo ni raha kukutana mara kwa mara na kutaniana kama desturi ya Wabongo.

Swali: Unafanya nini hasa?
Jibu: Shughuli yangu mahsusi ni uwakili na nimeshafanya kazi mbalimbali za kijumuiya kusaidia maendeleo kupitia mashirika ya kimataifa kama  CUSO (Canadian University Services Overseas).  Nilipofika hapa nilifanya  miradi mbalimbali  kusaidia wananchi toka Zimbabwe na Msumbiji. Baadaye nikafanya kazi na  cha RMIT kwa miaka 18 na  chuo cha Monash College.  Vyuo hivi vina hadhi sana hapa Australia.  Kimuziki nilijiunga na Waafrika wengi mara nilipofika. Nimeshapiga na Clan Swahili, Musiki Manjaro na sasa hivi niko na Public Opinion Afro Orchestra.

Swali: Tufafanulie kidogo kuhusu Public Opinion Afro Orchestra na CD yenu, “Do Anything, Go Anywhere”.

Jibu: Bonge la bendi huwa lina kati ya wanamuziki 17 hadi 21 toka Ghana, Malawi, Afrika Kusini, Namibia.  Tuliianzisha bendi miaka mitatu iliyopita; mimi nilikuwepo toka mwanzo.  Napiga gitaa, natunga, ninaimba na kuhusika na kila kitu.

Swali: Kwa hiyo mnapiga muziki ya Fela Kuti?
Jibu: Tunaendeleza Afro Beat lakini hatuishii hapo kama vikundi vingine duniani. Tunaongeza mapigo ya Hip Hop  na kuendeleza fikra zake marehemu Fela Kuti.

Swali: Vijana wengi Tanzania hawakufahamu maana unatoka Kizazi cha miaka ya Sabini kilichonguruma na muziki babu kubwa Bongo.

Jibu: Kweli miaka ya 1970’s ilihamasishwa na mitindo mbalimbali ya  Soul, Funk, Rock, Rumba, Afro Beat na wanamuziki mashuhuri duniani akina Jimi Hendrix, Beatles, Led Zeppelin, Wilson Pickett, James Brown, Aretha, The Temptations, George Benson, BB King, Franco, Fela Kuti, Lipua Lipua, Fauvette,  Buddy Guy, Sparks, Maquis du Zaire, Groove Makers, Tonics, NUTA Jazz, Rifters wote walipendwa na kuniathiri sana.  Nilianza kupiga gitaa nikiwa na miaka 11 mjini Arusha kisha nikaendelea Dar es Salaam nikiwa na miaka 16.  Nilipiga na bendi za miji hii miwili iliyoshiba muziki kama Funky Mob, Hijackers, Shades of Time, Comets, Sound of Hope, Watafiti na kuishia kuiongoza Tatu Nane kabla sijaondoka 1991.

Swali: Unashikwa huzuni ugenini?
Jibu: Ninaipenda Tanzania ni nchi niliyokulia na Malawi nilikozaliwa. Naihusudu Bongo na ukarimu wao.  Rais Nyerere ni shujaa wangu kwa jinsi alivyotusaidia wakimbizi tulioshukia hapa.  Niliotea na kutumaini hali ya kwetu Malawi ingebadilika lakini haikubadilika nikaamua kuhamia Australia kabisa na familia yangu. Hapa wanangu wanapewa elimu na serikali hii.  Haikuwa rahisi kuacha kula ugali, samaki wa kuchoma na nguvu za muziki wa Afrika.

Swali: Wanamuziki wengi wa Kiafrika wanaoishi ughaibuni wanalazimika kufanya kazi wasizotaka kama ufagizi, korokoroni badala ya kufanya shoo kama walivyotazamia kutokana na ugumu wa maisha.  Nini maoni yako?
Swali: Nimewaona wanamuziki wengi wakiwasili hapa Melbourne wakijitapa kwamba wao ni “Babu Kubwa,” lakini suala lililopo ni je unaweza kujenga jina?  Kinachohitajika ni nidhamu ya kazi, upeo wa mawazo, kufanya kazi kwa subira na wenzako katika bendi badala ya kujiona na kujifaragua.

Kama wewe ni mwanamuziki mzuri basi jenga jina nyumbani halafu ikiwezekana nenda miji kama New York ujulikane kama akina Richard Bona (Cameroon) Angelika Kidjo (Benin) and Lionel Loueke (Benin)…

Swali: Unauonaje muziki wa Kizazi Kipya kulinganisha na wa enzi zenu?
Jibu: Mimi mshabiki mkubwa wa Profesa Jay.  Ana maneno na fikra safi.  Uzuri wa Bongo Flava ni kwamba, wana maudhui mazuri kinyume na wenzao toka Kenya, ingawa siwashushui ndugu zetu hao.

Swali: Unauonaje muziki Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla?
Jibu: Afrika inashikilia dira ya maendeleo ya muziki wa dunia.  Waangalie akina Richard Bona, Hugh Masekela, Lionel Loueke, Angelika Kidjo na Waaafrika wengine mashuhuri wanavyotingisha na kuifanya dunia ijitizame upya kimuziki! Kwa Afrika Mashariki mi namzimia Prof Jay tu.

Swali: Kwa hiyo una matumaini makubwa kwa muziki wa Kiafrika?
Jibu: Ndiyo sababu naupiga muziki huu.  Nauamini na nina hakika tutafika mbali.

Swali: Je utawashauri vijana wa Kitanzania kwenda ng’ambo kujaribu bahati yao?
Jibu: Ndiyo. Kama unajua kazi usijivunge.  Ila kabla hujatoka chunguza utakwenda wapi, utafanya nini, uelewe biashara ya muziki ikoje; usiimbe tu Napaa Majuu bila mpango au kipaji.

Habari zaidi tembelea: http://www.thepublicopinion.net
Simu: +61-413-780-622
-London, 18 Januari, 2011.
-Barua pepe: kilimanjaro1967@hotmail.com
-Tovuti: http://www.freddymacha.com
Simu: +44-7961 -833040

 

 

12

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s