KIINGEREZA KITAANGAMIZA ZAIDI ELIMU YETU

Maggid Mjengwa

Maggid Mjengwa

MRABA WA MAGGID

Toleo la 336  MWANANCHI Tarehe 29 Mwezi wa Kwanza2014

IMERIPOTIWA kuwa baadhi ya shule za msingi hapa nchini zimeanza kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia.

Haya ni makosa makubwa kwa vile hatujawahi kuwa na maandalizi. Na kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia si jawabu, bali, kuongeza tatizo la uelewa wa wanafunzi wetu. Tujiulize; hilo litawezekana vipi wakati asilimia kubwa ya walimu wetu nao wanapata shida kwenye kutumia Kiingereza hata kwenye mazungumzo ya kawaida tu?

Tuache kujidanganya wenyewe. Hizi ni dalili za taifa la watu ambao sio tu hawajithamini wenyewe, bali pia hawajitambui. Kiswahili hiki ni zaidi ya lugha. Hakika, lugha yetu ya Kiswahili pia ni utamaduni wetu. Kuitangaza, kuikuza na kuilinda lugha yetu ya Kiswahili ni juhudi za kuulinda utamaduni wetu.

Hivyo, Kiswahili ni Utamaduni wetu. Na utamaduni ni utaratibu wa maisha ikiwa ni pamoja na  sanaa za maonesho, muziki asilia, ngoma za asili, tamthilia, lugha, sanaa za ufundi, filamu na chakula. Huwezi kuyapandikiza hayo kwenye vichwa vya watu kwa kutumia lugha ya kigeni.

Maana, utamaduni ni utambulisho wa mtu husika. Kama huwezi kuuthamini utamaduni wako, basi, umeshindwa kujithamini mwenyewe. Ni nani basi atakayekuthamini?

Tuna kila sababu ya  kujikita katika kurejesha heshima, hadhi, moyo na juhudi za kukuza utamaduni wetu unaotishiwa kumezwa na tamaduni za kighaibu hususan zile za kimagharibi. Tutumie  utandawazi unaoambatana na sayansi na teknolojia kama  nyenzo na fursa ya mafanikio ya jitihada za kuendeleza, kukuza, kusambaza na kuuza utamaduni wetu.Tuuthamini, kuuendeleza na kuukuza utamaduni wetu. Hii ni pamoja na lugha yetu ya Kiswahili.

Leo hii ukisikiliza muziki unaopigwa kwenye redio zetu, filamu zinazonyeshwa na hata kuigizwa na Watanzania wenzetu. Ukiangalia namna ya mavazi tunayovaa, vyakula tunavyokula na hata  lugha tunayozungumza. Vyote hivyo havitoi taswira ya utamaduni halisi wa Mtanzania. Maeneo ya mijini ndiyo yanayoelekea kumezwa zaidi na tamaduni za kighaibu.

Tuna haja ya kutafakari kwa kina juu ya utamaduni tunaoujenga sasa. Itakumbukwa,  miaka ile ya mwanzoni mwa uhuru wetu, masuala ya utamaduni yaliwekwa chini ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Wizara hii ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1962. Kunako Desemba 10, mwaka 1962, Mwalimu Nyerere aliweka bayana majukumu ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana, Mwalimu alitamka yafuatayo;  “Mabadiliko makubwa niliyoyafanya ni kuanzisha Wizara mpya ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Nimefanya hivyo kwa kuamini kuwa Utamaduni ni kitu muhimu na ni roho ya taifa lolote liwalo.

Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu walikosa hari na moyo wenye kuwafanya kuwa taifa. Moja ya dhambi kubwa ya wakoloni ni ile hali ya kutufanya tuamini kuwa hatuna utamaduni wetu wa asili; au kwamba yote tuliyokuwa nayo hayakuwa na thamani yeyote-kitu ambacho tulipaswa tukionee aibu badala ya kuwa chanzo cha kujivunia.

Baadhi yetu, hususan wale tulioelimishwa na Wazungu tunanajaribu kuwathibitishia wakoloni waliotutawala kwamba “tumestaarabika” ikiwa na maana tumeachana na yale yote yenye kutuunganisha na utamaduni wetu wa asili. Kwamba tumejifunza kuiga utamaduni wa Kizungu. Malengo ya vijana wetu hayakuwa kuwa Waafrika walioelimika bali kuwa Wazungu Weusi.”  Hayo ni maneno ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962.

Bila shaka, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mfano wa viongozi waliothamini na kuuenzi utamaduni wetu ikiwemo lugha ya Kiswahili. Leo tunashuhudia jinsi jamii yetu ilivyovamiwa na tamaduni za kighaibu. Ni dhahiri kuwa utamaduni unaimarika kwa kuiga yaliyo mazuri kutoka tamaduni nyingine.

Lakini, katika jamii yetu, tamaduni za kighaibu hususan kutoka Ulaya na Marekani zaelekea kukumbatiwa zaidi na wanajamii na hivyo basi kuhatarisha kuufifisha na pengine kuuangamiza utamaduni wetu.

Vijana wetu wanaona fahari zaidi kuimba na kucheza nyimbo na miziki ya kighaibu. Wanaona aibu kuimba nyimbo za Kiswahili. Nyimbo za makabila yetu kwa mfano  Kinyamwezi, Kizaramo na nyinginezo za asili. Vijana wetu wanaona fahari kuongea Kiswahili kwa lafudhi ya Kiingereza. Vijana wetu wengi wa siku hizi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kucheza Gombe Sugu, Mganda, Mangala, Konge, Nyang’umumi, Kiduo, au Lele Mama. Hizi ni baadhi tu ya ngoma zetu za asili. Vijana wetu wengi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kupiga vyombo vya muziki vya asili kama vile Marimba, Kilamzi, Ligombo au Imangala.

Na tuangalie ni jinsi gani tutaweza kuuhifadhi, kuuendeleza na kuuimarisha utamaduni wetu. Hivi leo kuna wanaozungumza au kuandika kwa Kiingereza mahali ambapo asilimia 90 ya wasikilizaji au wasomaji ni wazungumzaji wa Kiswahili. Hiyo ni hali ya kutojiamini. Ni kubaki katika hali ya utumwa wa fikra. Je, wenye kufanya hivyo wana malengo ya kuwaonesha “wakoloni” au “Wafadhili” wa semina kwamba wao “Wamestaarabika”? Au wanafanya hivyo ili kuwaridhisha Wafadhili tu? (Rejea kauli ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962 hapo juu). Kwa nini waandaaji wa semina wasitumie wakalimani kuwatafsiria wasio wazungumzaji wa Kiswahili ambao ni asilimia kumi tu ya kadamnasi. Hilo pia lingetengeneza ajira kwa baadhi ya Watanzania. Tubadilike.

Wasiliana na mwandishi

Maggid Mjengwa

mjengwamaggid@gmail.com

+255-754678252, +255-712956131

http://mjengwa.blogspot.com

Maggid Mjengwa pia ni Mwandishi wa Kitabu; “Maisha Ya Barack Obama, alikotoka, aliko na anakokwenda”. Kinapatikana mitaani.

 

 

Maoni ya Wasomaji

Wakati mwingine tuwe wakweli

Permalink Submitted by Msomaji wetu (not verified) on Sun, 2014-02-02 02:14.

Wakati mwingine tuwe wakweli na tuache siasa. Leo tunasema tutumie Kiswahili kufundishia hadi vyuo vikuu halafu bado tunalalamika kuwa kazi zetu zinachukuliwa na wakenya, waganda na sasa warwanda. Bado hatufanyi juhudi angalau tufundishe watoto wetu kiingereza ili waweze kushindana na wengine na waweze kupata kazi nzuri. Mimi ni shabiki mkubwa wa blog na makala yako lakini kwa hili umekosea bwana mjengwa. Na imani kuwa watoto wako wanasoma English academy na pia pengine wanafahamu na lugha nyingine zaidi ya English na Kiswahili. Hao mnaowaita viongozi wenu wanapeleka watoto wao kwenye shule za kimataifa zilizopo huko TZ na pia nchi za nje halafu wanawaambia ninyi maskini msipeleke watoto wenu shule nzuri ili wasipate elimu nzuri kuweza kushindana nao. Msiwe wajinga watanzania…hatufanyi vizuri kwenye job competition kwa sababu hatuna advanced knowledge ya English kulinganisha na ya majirani zetu, tunasema tuna utamaduni wa Kiswahili lakini mngejua huku nje inajulikana Kiswahili kinatokea Kenya mngeshangaa, Wenzetu hao ni wajanja…ndiyo hawajui Kiswahili vizuri lakini wanatumia kiingereza wanachokijua vyema kusambaza propaganda za kuwa Kiswahili ni chao wakati sisi tumelala.

Wakati muda mfupi kabla

Permalink Submitted by Msomaji wetu (not verified) on Tue, 2014-02-04 13:42.

Wakati muda mfupi kabla sijayasoma makala yako, rafiki yangu kanipigia simu huku akitetemeka kwa hasira. Kisa, mwanaye kapewa adhabu ya kuwa nyumbani kwa wiki mbili kwa kosa la kuimba shairi la Kiswahili. Maoni yangu ni kuwa tangu zamani mtu kujua zaidi ya lugha moja ni fursa.

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s