MCHANGO WA KIINGEREZA KATIKA KUDIDIMIZA MAENDELEO YA ELIMU NCHINI

 Faraja Kristomus Na Faraja Kristomus

Part one

Hii ni Wiki ya Elimu nchini ambayo Kauli Mbiu yake ni « Elimu kwa wote inawezekana, timiza wajibu wako ». Naipongeza serikali kwa uamuzi huu wa kuwa na wiki ya elimu kwa ajili ya kuwakutanisha wadau wa elimu ili waweze kujadili changamoto za elimu nchini.

Lakini leo ningependa kusema wazi kuwa kwa viko vikwazo vingi vinavyowafanya Watanzania wasipate haki hii ya elimu nchini. Sidhani kama kauli mbiu hii inalenga kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi walioko mashuleni bali kuwa na tafsiri pana ya elimu.

Inaposemwa elimu kwa wote inawezekana inamaanisha kuwa watoto wanaoenda shuleni basi wapate maarifa yatakayowafanya wawe wananchi bora na wanufaike na elimu wao na vizazi vijavyo. Kwa bahati mbaya Watanzania wengi wamenyimwa fursa ya kupata elimu ingawa wamekuwa wakihudhuria madarasani.

Haki hii ya kupata elimu imekosekana kwasababu katika ngazi ya sekondari wanalazimika kujifunza kwa Kiingereza ambacho kwa bahati mbaya hawana msingi nacho mzuri wakati wa kumaliza darasa la saba. Na wanaendelea kukosa maarifa kwa sababu ya kikwazo cha Kiingereza hadi wanapofika chuo.

Nianze kwa kutetea hoja yangu kwa kuanzia na matokeo ya utafiti wa uwezo wa mwaka 2012. Ripoti ya utafiti huo inaonyesha kuwa ni asilimia 53 tu ya watoto walioko darasa la saba ndio walioweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili. Hii inamaanisha kuwa ni watoto watano kati ya kumi ndio wanaomaliza darasa la saba wakiwa na uwezo walau wa kusoma hadithi rahisi ya Kiingereza.

Hata hivyo ufaulu huu wa Kiingereza unatofautiana kimikoa hapa nchini. Kwa maeneo ya mijini ufaulu wa Kiingereza ni mzuri zaidi kuliko maeneo ya vijijini. Utafiti huo wa uwezo wa 2012 unataja wilaya ambazo watoto wake waliongoza kufeli Kiingereza kuwa ni Kasulu, Handeni, Urambo, Biharamulo na Serengeti.

Na katika wilaya tano zilizoongoza kwa kuwa na watoto waliofanya vizuri, nne ni za mjini na moja ni ya vijijini lakini ikiwa karibu zaidi na mji. Wilaya hizo ni Arusha Mjini, Moshi Mjini, Songea Mjini, Arusha Vijijini, na Morogoro Mjini.

Lakini cha kusikitisha ni kwamba wilaya iliyoongoza kwa watoto kufaulu Kiingereza, bado kiwango cha kufaulu ni asilimia 55 tu na wilaya ya tano ambayo ni Morogoro Mjini walifaulu kwa asilimia 46.2. Hii inatupa picha kuwa utafiti huu unaendana na uhalisi wa ufaulu wa Kiingereza kwa mwaka 2013 ambapo asilimia 35.5 ilikuwa ya wastani wa ufaulu kwa Kiingereza.

Kwa kuangalia takwimu hizi utaona kuwa upo uwezekano mkubwa kuwa watoto wanaosoma shule za mjini wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri kimasomo kuliko watoto wanaosoma shule za vijijini.

Utafiti wa uwezo unatupa picha ya jinsi tatizo la kiingereza lilivyo kubwa kwa wanafunzi wetu kiasi ambacho linatishia ufanisi wa wanafunzi wawapo sekondari ambako Kiingereza kinatumika kama lugha ya kufundishia. Wanafunzi wengi wanajiunga na kidato cha kwanza wakiwa hawana msingi mzuri wa Kiingereza.

Hili linadhihirishwa na matokeo ya Kiingereza ya darasa la saba kwa mwaka 2013. Wanafunzi waliofaulu Kiingereza mwaka 2013 walikuwa asilimia 35.5 tu. Hata hivyo ufaulu huo uliongezeka ukilinganisha na asilimia 21.06 ya wale waliofaulu mwaka 2012.

Kwa maneno mengine ni kwamba idadi kubwa ya watoto wanaoenda sekondari bado wanakuwa na tatizo la Kiingereza;lugha ambayo inatumika kuwafundisha karibu masomo yote isipokuwa Kiswahili.

Kwa hiyo katika makala haya nitajikita zaidi katika kuelezea kwa nini kuna shida katika ufaulu wa Kiingereza na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kwa sasa.

Ukipitia silabasi ya kiingereza ya shule za msingi utaona kuwa hakukuwa na sababu ya mtoto anayemaliza darasa la saba asijue Kiingereza kwa ufasaha. Endapo kila kilichomo humo kingefundishwa basi tungeweza kuwa na vijana ambao wanamaliza shule ya msingi wakiwa na uwezo mkubwa wa kujieleza kwa Kiingereza.

Mbali na silabasi, bali pia muda ambao umetengwa na wizara ya elimu kwa ajili ya kufundisha Kiingereza ungetosha sana kumwandaa mtoto ajue Kiingereza.

Siku za masomo au za shule kufundisha ni 194. Kwa wiki nzima mwanafunzi wa darasa la kwanza na la pili anapaswa kusoma Kiingereza kwa dakika 210 yaani saa tatu na nusu. Mwanafunzi wa kuanzia darasa la tatu hadi la saba anapaswa kufundishwa Kiingereza kwa saa nne na nusu kwa wiki.

Kiwango cha chini kinachokubalika na wizara cha kufundisha Kiingereza kwa mwaka mzima wa masomo ni kuanzia saa elfu kumi kwa darasa la tatu hadi darasa la saba na saa 7500 kwa darasa la kwanza na la pili. Kwa mantiki hii, endapo Kiingereza kingefundishwa kwa umakini basi tungekuwa na wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza wakiwa na uwezo mkubwa wa kuelimika.

Katika makala zitakazofuata nitaongelea zaidi kuhusu mbinu za ufundishaji wa Kiingereza na matatizo yake na jinsi zinavyochangia kudumaa kwa maendeleo ya Kiingereza nchini.

Advertisements

2 thoughts on “MCHANGO WA KIINGEREZA KATIKA KUDIDIMIZA MAENDELEO YA ELIMU NCHINI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s