SHULE YA MSINGI MPAGO: UFAULU MZURI CHINI YA MITI

Shule ya Msingi Mpago“Shule hii ilianza mwaka 2007 ikiwa imesajiliwa kwa namba KA 0503207  ikiwa na jengo la madarasa haya mawili. Baadaye wanakijiji wamekuwa wakipambana kuendelea kujenga madarasa. Lakini mwaka 2012, walikuja Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na kusema kuwa kijiji kiko ndani ya hifadhi.’’

Na Elias Msuya, Mwananchi Posted  Jumanne, Tarehe 3 Mwezi wa Sita  2014  saa 12:27 PM

KWA UFUPI

Wahitimu wa kwanza wa shule hiyo mwaka jana walikuwa 42, wakafaulu wanafunzi 39.

Unapofika katika kijiji cha Mpago kilichopo wilayani Biharamulo huwezi kuamini kama kuna shule hadi utakapoona wanafunzi waliovaa sare.

Kijiji hicho, kilichopo wilayani Biharamulo, umbali wa kilometa 15 kutoka barabara itokayo Kahama mkoani Shinyanga kwenda mikoa ya Kagera na Kigoma, kinapakana na hifadhi ya msitu wa Nyantakara.

Sasa kijiji hicho kimeingia kwenye mgogoro na Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) unaodai kuwa kiko ndani ya mipaka ya msitu huo.

Mgogoro huo umedhoofisha maendeleo ya elimu kijijini hapo kiasi cha kuifanya Shule ya Msingi Mpago kukosa majengo ya kutosha, hivyo kuishia kuwa na madarasa mawili na la tatu halijakamilika.

Hata hivyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mukiza Sebastian anasema licha ya kuwepo kwa mgogoro huo, bado wanafanya kazi kwa bidii na mafanikio yanaonekana.

“Shule hii ilianza mwaka 2007 ikiwa na namba KA 0503207 ya usajili wakati huo jengo lake lilikuwa na madarasa mawili. Baadaye, wanakijiji wamekuwa wakipambana kuendelea kujenga madarasa kwa kujitolea,” anasema Sebastian.

“Lakini mwaka 2012, walikuja TFS na kusema kuwa kijiji cha Mpago kiko ndani ya hifadhi hivyo kitahamishwa, ndiyo maana hata ujenzi wa madarasa umesimama.”

Anaendelea kusema kuwa kwa kuwa wanafunzi wamekuwa wakiongezeka kila mwaka na wanalazimika kuwafundishia chini ya miti.

“Pamoja na kusimamisha ujenzi wa shule, bado Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo inaendelea kutupa walimu, ruzuku na vitabu,” anasema Sebastian na kuongeza kuwa shule hiyo kwa sasa ina walimu saba wote wanaume na wanafunzi 418.

“Wanafunzi wa darasa la saba na la kwanza ndiyo wanaotumia madarasa haya mawili wengine wote wanasomea chini ya miti. Walimu wote ni wa kiume, inawezekana Serikali imeona mazingira haya hayafai kuleta walimu wa kike,” anasema.

Maendeleo kitaaluma

Licha ya changamoto hiyo, mwalimu wa taaluma, Twimanye Kasaba anasema shule hiyo iliyotoa wahitimu wa kwanza mwaka 2013 imefanya vizuri.

“Tumeshika nafasi ya 17 kati ya shule 78 kwa Wilaya ya Biharamulo, shule ya 70 kati ya 903 za Mkoa wa Kagera na shule ya 479 kati ya 15,656 kitaifa,” anasema Kasaba na kuongeza:

“Pamoja na kusomea nje, wanafunzi wana mwamko mkubwa wa elimu, ndiyo maana mwaka jana kati ya wahitimu wa kwanza waliokuwa 42, 39 walifaulu na kwenda sekondari.”

Anaendelea kufafanua kuwa, kinachosababisha mafanikio hayo ni moyo wa kujituma walionao walimu huku wanafunzi ambao nao wanaoishi katika mazingira magumu kijijini hapo wakionekana kujituma.

“Elimu ni walimu na wanafunzi, hayo mengine ni nyongeza tu. Sisi kama walimu tumeajiriwa kufundisha hivyo haturudi nyuma,” anasema.

Anaongeza: “Ni kweli, nyakati za mvua huwa ni ngumu sana kwetu, lakini tunajitahidi kuwarundika tu wanafunzi kwenye hayo madarasa mawili. Kwa mfano, darasa la kwanza, pili na la tatu tunawaweka chumba kimoja na madarasa ya nne, tano, sita na saba darasa jingine. Kama mvua ikizidi tunawafundisha humo humo kwa zamu.”

Kiini cha mgogoro

Akifafanua kiini cha mgogoro kati ya kijiji cha Mpago na TFS, Mashauri Paschal, ambaye ni diwani wa Kata ya Kaniha, anasema ulianza mwaka 2012 baada ya wakala huo kuweka mipaka ya misitu na kudai kuwa kijiji hicho kimo ndani ya hifadhi.

Kata ya Kaniha ina vijiji vitano ambavyo ni Kaniha, Mpago, Msalabani, Mavota na Mukunkwa.

“Si kweli kwamba kijiji cha Mpago kimo ndani ya msitu wa Nyantakara kwa sababu, mpaka halisi upo kati ya mpaka unaotenganisha Mikoa ya Kagera, Shinyanga na Kigoma ambapo kuna mto,” anasema Pascal.

“Mpaka huo ulijengwa enzi za ukoloni mwaka 1943 na mzungu aliyekuwa akiitwa Hamilton akishirikiana na mwenyeji Simon Mkondo hadi sasa yupo hapa kijijini.”

Anaendelea kusimulia kuwa, katika mwaka huo, kulitokea janga la ugonjwa wa malale unaosababishwa na wadudu aina ya ndorobo.

“Bwana Ndorobo kutoka serikali ya kikoloni aliyejulikana kwa jina la Pare, alitumwa kuja kutathmini hali hiyo, ndipo akaweka mpaka wa eneo lililoathirika hadi katika kijiji cha Kaniha. Hivyo kijiji cha Mpago wakati huo kikiwa kitongoji kikawa ndani ya eneo la karantini,” anasema Pascal.

Pascal aliyezaliwa katika kijiji cha Kaniha mwaka 1953 anasisitiza kuwa mpaka unaogombewa na TFS ni ule wa karantini ya ndorobo.

“Baba yangu mzazi alizaliwa katika kijiji cha Kaniha mwaka 1921 na kuna wazee wapo hadi leo waliokuwa wakilipa kodi katika kijiji hiki miaka ya 1936. Wote hao wanao ushuhuda kuwa Mpago halikuwa eneo la hifadhi ya misitu. Kwa nini Serikali ya wilaya haitaki kuja kuwauliza na vielelezo vipo?” anahohoji.

Anafafanua kuwa, wakati wa ukoloni Kata ya Kaniha ilikuwa katika Jimbo la Tabora, baada ya uhuru ikahamishiwa Mkoa wa Shinyanga na mwaka 2010 ikahamishiwa wa Mkoa wa Kagera katika wilaya ya Biharamulo.

“Kwa nini walipotuhamishia Wilaya ya Biharamulo ndiyo watusumbue hivi? Kwa nini Serikali itoe usajili kwa kijiji cha Mpago mwaka 2010 halafu leo ije tena idai kuwa kijiji hicho kimo hifadhini?”

“Unapomnyang’anya mwanakijiji shamba lake kwa kudai kuwa liko hifadhini, unatarajia nini kwa maendeleo yake na maendeleo ya elimu ya watoto wao yatakuwaje?” anahoji.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Zephania Chandika anasema wanapambana kukitetea kijiji chao.

“Ni kweli kijiji chetu kimesajiliwa kwa namba KGR KIJ 695, lakini tangu mwaka 2012 TFS walikuja hapa na kudai kuwa tuko ndani ya hifadhi,’’ alisema.

Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Paulina Ndegeza anakiri kulifahamu suala hilo na kwamba limeshajadiliwa katika ngazi ya wilaya, mkoa na kupelekwa ofisi ya Waziri Mkuu.

“Hilo suala tunalifahamu, tumeshalijadili sana, lakini tumeamua tulifikishe kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa uamuzi wa mwisho. Kwa sasa sisi kama halmashauri hatuwezi kulizungumzia tena,” anasema Ndegeza

“Tunaendelea kutoa huduma za elimu kwa kuwa bado kule kuna wananchi na wanahitaji hizo huduma.”

Advertisements

One thought on “SHULE YA MSINGI MPAGO: UFAULU MZURI CHINI YA MITI

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s