WAMPIGISHA KWATA WAZIRI WA AFYA

Dk. Seif Rashid, Waziri wa Afya

Dk. Seif Rashid, Waziri wa Afya

Na Fidelis Butahe na Sharon Sauwa, Mwananchi Posted  Alhamisi, Tarehe 5 Mwezi wa sita  2014  saa 24:0 AM

KWA UFUPI

“Kwa nini Bunge lilipitisha Sh753 bilioni wakati likijua wazi kuwa haziwezi kupatikana, Watanzania watapataje huduma za afya?”.

  1. Wabunge wanawake bila kujali itikadi za vyama juzi usiku waliungana kuibana Serikali wakishinikiza iongeze fedha za Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ya mwaka 2014/15 ili kukabiliana na vifo vya kina mama na watoto.

Kibano hicho kilianza mapema asubuhi lakini moto zaidi uliwaka jioni wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti hiyo iliyotengewa Sh622 bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/14 ambayo ilitengewa Sh753 bilioni. Wabunge wanawake 10 na wanaume wawili walichangia ikiwamo kutoa shilingi.

Kambi ya Upinzani ilianza kuibana Serikali ikisema imeweka rehani wananchi wake kutokana na kitendo chake cha kuchangia kiasi kidogo cha fedha za maendeleo za wizara hiyo.

Akiwasilisha taarifa ya kambi, Waziri Kivuli wa Afya, Dk Anthony Mbassa alisema Bajeti ya Sh622 bilioni na fedha za maendeleo ni Sh305 bilioni ambazo kati ya hizo, Serikali itatoa Sh54 bilioni tu, wakati washirika wa maendeleo watatoa Sh251 bilioni.

“Hii inaonyesha wazi kuwa Serikali imeendelea kuweka rehani wananchi wake kutokana na bajeti kuendelea kuwa tegemezi kwa wahisani,” alisema.

Kibano cha wanawake

Licha ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima kutoa ufafanuzi, walishindwa kuwashawishi wabunge hao waliokuwa wakililia nyongeza ya bajeti.

Hoja hiyo, iliibuliwa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Paresso baada ya kuondoa shilingi akiitaka Serikali itoe majibu ya sababu za kutoa Sh387 bilioni pekee kati ya Sh753 bilioni za bajeti ya mwaka 2013/14, jambo ambalo limekwamisha utendaji kazi wa wizara hiyo, ikiwa ni pamoja ya kushindwa kutekeleza Azimio la Abuja kuwa kila nchi itenge asilimia 15 ya bajeti kuu kwa ajili ya Wizara ya Afya ili kunusuru vifo vya kina mama na watoto.

Baada ya kauli hiyo wabunge kadhaa walisimama na kuunga mkono hoja hiyo licha ya Mwigulu kulieleza Bunge kuwa Serikali imepanga kuongeza kiasi cha fedha kilichobaki kabla ya Juni 31, mwaka huu.

Hoja hiyo ilifafanuliwa na Malima ambaye alisema Serikali imetoa Sh12 bilioni na kwamba tayari fedha hizo zimeshaingizwa katika akaunti ya Wizara ya Fedha kwa ajili ya kulipia deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ambalo ni Sh89 bilioni na deni la matibabu nje ya nchi ambalo ni Sh21 bilioni.

“Kwa nini Bunge lilipitisha Sh753 bilioni wakati likijua wazi kuwa haziwezi kupatikana, Watanzania watapataje huduma za afya?” alihoji Paresso.

Jaji Werema alijibu akisema Azimio la Abuja ni la hiari na hata kama nchi husika ikishindwa kulitekeleza haitapata adhabu yoyote, huku akisisitiza kuwa Serikali haikupata fedha za kufikia malengo ya azimio hilo na kuahidi kuwa kiwango cha fedha kilichobaki kitaongezwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.

“Serikali isiende nje ya mstari, hoja ya Paresso ni ya msingi, wizara inatakiwa kutoa majibu ya kueleweka kutokana na kuongezeka kwa vifo vya kina mama, Serikali ina vipaumbele vipi,” alihoji Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Maria Hewa na kuongeza:

“Eti mnasema mtapata fedha wakati zimebaki wiki mbili kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha, mtazitoa wapi? Wenzangu wote tukubaliane katika hoja hii bila kujali tofauti, kina mama wanavuja damu.”

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Pauline Gekul aliunga mkono hoja hiyo na kusema: “Fedha za MSD za kununulia dawa mwaka huu ni Sh45.8 bilioni wakati bohari hiyo inahitaji Sh250 bilioni… Fedha za vifaatiba zimepungua kwa kiasi cha Sh2.6 bilioni mwaka jana na mwaka huu ni Sh2.2 bilioni…”

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Esther Matiko alisema: “Jaji Werema anasema kuwa watazilipa, hilo haliwezekani. Ripoti ya CAG imeeleza kuwa Serikali inalipa mishahara hewa Sh1 trilioni, hizo fedha si zingeweza kusaidia bajeti hii. Huko vijijini hali ni mbaya tusaidieni kina mama tunakufa.”

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Mary Mwanjelwa alisema: “Hatuwezi kuwa na sauti ya kuongea kama hatuna afya. MSD hakuna dawa sababu wanaidai Serikali, wanawake jamani tuungane humu ndani sisi ndiyo tuna uchungu wa kuzaa watoto. Jaji Werema ni shemeji yangu lakini sikubaliani naye.”

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Zaynabu Vullu akaongeza: “Hatuko tayari kuona wanawake wakifa wakati Rais Jakaya Kikwete ametoa tamko kwamba vifo vya kina mama na watoto wakati wa uzazi vinapungua. Azimio la Abuja hatujalitekeleza, leo mnasema azimio hilo la hiari ili iweje?”

Mbunge wa Same Mashariki (CCM), Anne Kilango Malecela alieleza kusikitishwa na kitendo cha kuendelea kupungua kwa bajeti ya maendeleo ya wizara hiyo na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Margaret Sitta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii alisema: “Kamati haikuridhika na fedha zilizotengwa na tulipendekeza Sh100 bilioni ziongezwe kununua dawa na vifaatiba.”

Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu alimtaka Lukuvi kutoa maelezo ya kina baada ya wabunge hao kuchachamaa.

Lukuvi alisema Kamati ya Huduma za Jamii imeshaijadili bajeti ya wizara hiyo na kutoa ushauri na kwamba Waziri wa Fedha ameshaieleza kamati hiyo jinsi ilivyoongeza fedha.

Wakati Lukuvi akitoa maelezo hayo wabunge walikuwa wakiguna na kuonyesha kutokukubaliana naye na hivyo kumlazimu Zungu kuingilia kati kuwatuliza.

Paresso alipingana na maelezo ya Lukuvi na kuendelea kushikilia shilingi, akisisitiza kuwa hoja yake haikulenga bajeti ya mwaka 2014/15, bali ya mwaka 2013/14.

“Hoja yangu ni lini Serikali itakamilisha fedha za Wizara ya Afya kwa mwaka huu wa fedha unaoisha Juni 30? Kwa sababu mpaka Mei mwaka huu imepelekwa Sh387 bilioni kati ya Sh753 bilioni.

Akifafanua suala hilo, Dk Rashid alisema kati ya Sh753 bilioni za bajeti hiyo, Sh471.2 bilioni zilikuwa fedha za maendeleo ambazo wahisani waliahidi kuchangia Sh435 bilioni na Serikali Sh36 bilioni na kwamba fedha za wahisani Serikali haina madaraka nazo.

Nyongeza na Julius Mathias

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s