ABIRIA

Profesa Pete M. Mhunzi

 

Y.W.C.A., Nairobi ilikuwa kama nusu maili kutoka hoteli ya GREEN VIEW ambako nilisindikizwa na mwalimu wangu wa kwanza wa Kiswahili baada ya kuwasili Jomo Kenyatta Airport katika safari yangu ya kwanza kwenda Afrika. Mwaka ulikuwa 1973. Naye mwalimu jina lake Paul Mulwa Sumbi alikuwa anarudi baada ya miaka kumi na mmoja masomoni Marekani. Nilibahatika kukutana na wasichana wawili Wakenya huko mjini New York ambako walikuwa wanafanya kazi katika Ubalozi wa Kenya, Umoja wa Mataifa. Walinihurumia hali ya upweke niliyobashiri itakuwa inanikaribisha Nairobi wakanipa majina ya marafiki zao wawili pamoja na nambari ya simu na makazi yao yakawa Y.W.C.A. Basi baada ya kupangua na kupanga chumbani Green View nikawapigia simu urafiki uanze. Tukajulikana wenyewe kwa wenyewe tukapatana katika urafiki wa karibu. Ikawa kawaida yetu kila wikindi kwenda sinema kula chakula cha jioni na kutembea mjini Nairobi tukipitia Uhuru Park, Jomo Kenyatta Avenue na kwingineko.
Katika Y.W.C.A. kulikuwa na utaratibu wa kupokea wageni waliokuja kuwatembelea wasichana waliokaa pale. Baada ya kuingia sebuleni sehemu ya mapokezi inakabili anayeingia na ndani yake mama mmoja au wawili wakiwa tayari kusikiliza sababu iliyomfikisha mgeni. Baada ya kusalimiana inabidi mgeni amwulizie mkazi anayetafutwa. Naye mama angeomba mgeni amsubiri mkazi halafu kumpigia simu na kumwarifu mkazi mgeni anamsubiri. Ndivyo nilivyozoea kukutana na marafiki zangu nyakati za wikindi.
Baada ya muda wa mwezi mmoja au zaidi kupita na mimi kuzoeana na marafiki katika urafiki wetu, nilizoea kukutana naye msichana mmoja pale sebuleni nikiwasubiri marafiki zangu. Hatukusalimiana wala kutupiana jicho bali bila shaka tukatambuliana. Nilihisia maringo na ugomvi kutoka kwake. Kila tulipokuwa sebuleni alikuwa peke yake akifunikwa katika hali ya kuwepo mbali na tulipokuwepo. Alikuwa msichana wa maringo yanayozidi katika hali ya usumbufu usioweza kusalimishwa. Usoni tabasamu ni ngeni huenda haijafika isipokuwa makunjo yanayoharakisha aonekane ameshazeeka pasi na watoto sembuse wajukuu. Mrefu katika urefu uliopandisha pua juu ya mdomo ambamo utamu haujawahi kufurahishia ulimi kavu. Sura yake aliyojaliwa nayo na Mwenyezi Mungu imefunikwa na taswira ya kubuniwa na msanaa wa uchawi. Mdomo jeraha ya kisu alama yake damu. Nyusi zisizo na unywele kichoro cha makaa. Kope za bandia hapana unyewele ndizo zimebandikwa na guni. Mashavuni mumepakwa rangi nyekundu hasa yakijumlishwa na mdomo anaonekana mwenye sura ya damu damu. Akijitazama kiooni shetani anaibuka!
Siku moja alinijia nilipokaa katika subira ya waje marafiki twende zetu. Akanisalimia katika Kimombo chake chenye kujivuna na kujitenga na mtu kama mimi mpenda Kiswahili. Nami ninatafsiri: “Naomba radhi najua mimi na wewe hatufahamiani lakini tumeshaonana mara nyingi hapa sebuleni. Sina budi nikwambie ukweli niliyonayo juu yako. Wewe ni mjinga kuwashinda wajinga wote waliokutangulia katika maisha ya binadamu duniani humu. Nimekutazama mara nyingi najua wewe ni Mmarekani uko matembezini. Lakini mbali na watalii wengine wanaokuja Afrika wewe unatafuta urafiki na wenyeji! Watalii kawaida wanafuata wanyama kwenye mibuga yao ila wewe, mbumbumbum wa aina yake! Ulipita nchi za Ulaya kuja Afrika! Umelipa gharama zaidi tikiti bei yake ghali zaidi kuliko ya kwenda nchi za Ulaya. Mjinga wewe! Mjinga sana!”

Nikashtuka sijui la kusema kisha nikajikaza kisabuni na kumjibu. “Nakuhurumia umeshindwa kufurahia Nairobi pengine Afrika nzima lakini umenipima nafsi ilivyo barabara! Mimi nashukuru Mungu nimewahi kuja Afrika na kukutana na watu wazuri wachangamfu ambao wamenikaribisha kama ndugu aliyepotea hajui ametoka wapi.
Sasa naomba nikweleze zaidi furaha inayonijaza moyoni kweli kusikia laa ndani ya loo! Mimi na wewe hukutana nyakati za wikindi ninapokuja kufuata marafiki zangu hapa Y.W.C.A. kwa sababu hao wanafanya kazi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa. Ndizo nyakati hizo raha inazidi kwangu! Wajua asubuhi na mapema siku hizo hizo kuanzia saa mbili hivi hadi mbili u nusu mabasi yamejaa abiria kila mtu anaenda kazini. Mimi huamka asubuhi na mapema, nakimbilia kituo cha basi kusubiri kama wengine wanaoenda kazini. Basi ikija abiria wanajitupa ndani hali ya mkukumkuku wakitafuta viti. Wengine wasiowahi viti inabidi wasimame wakishika kamba za juu. Ila yangu, mimi sitaki kuketi nakusudia kusimama; kwani ndipo raha hunipandisha juu kufikia kilele cha ulevi usio na changaa wala kukumoshi! Mimi husimama nikishika kamba ya juu na kunusanusa makwapa ya akina dada!
Raha mustarehe!
Laa ndani ya loo!”
Yule akageuka akaenda zake sijui kama tulionana tena.
Na Pete M. Mhunzi
31 Mwezi wa Nane 20013

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s