KASUMBA YA LUGHA ZA KIGENI INAVYOATHIRI MAANDIKO YA KISWAHILI

Stephen Maina

 

MSIMAMO, Tarehe 24 Mwezi wa Nane 2012

Na Stephen Maina
TUNAPOANDIKA makala au taarifa kuhusu matukio mbalimbali yaliyojiri katika jamii, kwa mujibu wa sarufi ya Kiswahili, ni muhimu tutunge sentensi ambazo zinatumia maneno kwa utaratibu maalumu.

Utaratibu huu ni wa kutumia maneno ambayo yanatakiwa yaoane na viambishi ili sentensi iwe na mantiki.

Mara kwa mara makosa ya kisarufi hujitokeza kutokana na kutozingatia utaratibu wa muundo wa Kiswahili kwani ni wa kipekee kabisa.

Kwa maana hiyo, tunapozungumza au tunapoandika Kiswahili, hatuna budi kujiweka katika mazingira ya Kiswahili.

Wako wale ambao wana kasumba ya lugha za kigeni waliozoea kuandika kwa kutumia fikra zilizoathiriwa na dhana za kigeni au za asili, wanatakiwa kujirekebisha na wajirudi kwani wanafikiri kwa misingi ya Kiingereza na kuandika kwa kutumia maneno ya Kiswahili.

Baadhi yetu tunafanya hivyo ama kwa kutofahamu kuwa tunakosea au kutokana na kasumba kwa maana ya kuzidiwa kwa athari ya lugha za kigeni.
Kwa ufafanuzi angalia sentensi zifuatazo:

“Baada ya kusikia mwanangu ameanguka na kuumia, nilidamka mara moja bila hata ya kuosha uso na kumpeleka zahanati kwa matibabu.”

Kwa mawazo ya haraka haraka, itaonekana kuwa sentensi hii ni sahihi lakini sivyo. Neno lenye walakini ni ‘kuosha’. Kuosha ni kusafisha kitu, mara nyingi kwa kutumia maji. Kama tunataka kufanya usafi wa uso kwa kutumia maji, tunanawa uso.

Vilevile, kama tunataka kufanya usafi wa mwili, tunaoga mwili. Pia, kama tunataka kufanya usafi wa nguo, tunafua nguo. Kwa bahati mbaya wasomi huweza kufasiri neno hilo kuwa ni ‘wash’.

Neno ‘wash’ kwa dhana ya kigeni inatafsiriwa kama kunawa uso, kufua nguo na pia kusafisha kitu. Kwa hiyo inabeba maana ya nguo, chombo/kitu na uso.

Mfano mwingine:

Kuna wakati iliwahi kuandikwa na kusomeka kama ifuatavyo:

“Kutafanyika sherehe ya kumbatiza mtoto katika Ukumbi wa New Palace Hoteli na wote mnatakiwa kuhudhuria bila kukosa.”

Mfuatano wa maneno New Palace Hoteli ni muundo wa Kiingereza na ilitakiwa kuandikwa “Hoteli ya New Palace.” Mara nyingi baadhi yetu tunaandika hivyo. Pia, tunapotoa mwaliko tunasema,“mnaombwa kuhudhuria au tafadhali usikose kuhudhuria .”

Tunaposema wote mnatakiwa kuhudhuria, tunakuwa na tafsiri ya “you are asked to au you are required to’. Miundo hii inatufanya tutoke katika mifumo ya utamaduni wa Kiswahili na kuingia katika mfumo wa lugha za kigeni.

Tatizo ninaloliona hapa ni kutafsiri neno badala ya dhana iliyopo. Sasa tuangalie makosa mengine katika magazeti ya Kiswahili.

“Kaka amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu ya AC Milan ambayo aliowahi kuichezea kwa muda wa miaka sita kabla ya kujiunga na Real Madrid.”

Kuandika ‘ambayo aliowahi’ kuichezea ni makosa ya kisarufi. Itabidi ama kuondoa ‘ambayo’ au kurekebisha tahajia ya ‘aliowahi’ lakini siyo kuandika maneno yote kwa pamoja kwa mfuatano kama ilivyo hapo juu.
Isomeke, “ Kaka amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu ya A C Milan ambayo aliwahi kuichezea kwa muda wa miaka sita kabla ya kujiunga na Real Madrid.
”Au “Kaka amekuwa akihusishwa na kuhamia klabu ya A C Milan aliyowahi kuichezea kwa muda wa miaka sita kabla ya kuijunga na Real Madrid.”

“Haishangazi kuona baadhi ya kampuni za uchimbaji madini, simu, hoteli na mengineyo kuwa leo hayalipi kodi licha ya kuvuna rasilimali kubwa za Watanzania.”

Tukitumia neno kubwa tuna maana kuwa ni kivumishi na maana yake ni kuzidi kiwango au kimo. Kwa kawaida rasilimali ni nyingi na wala siyo kubwa. Haina maana kusema kuwa wanavuna rasilimali kubwa. Vilevile hoteli huwa nyinginezo na wala siyo mengineyo kwa mujibu wa taratibu za kisarufi.

Katika kichwa cha habari kwenye gazeti moja mashuhuri hapa nchini iliwahi kuandikwa:
“Wadada Canada wawazima Waingereza.”

Haya ni maelezo yaliyoandikwa kuonyesha kuwa wasichana wa Canada wamewashinda wale wa Uingereza.
Kimsingi, neno dada halina wingi. Dada anakuwa mmoja na kama ni wengi tunaendelea kuandika dada. Uko mtindo ulioenea kwa wazungumzaji wengi hasa wa Jiji la Dar es Salaam wanaopenda kutumia neno dada na kuongeza mbele yake kiambishi /m/ na hivyo kuwa mdada.
Vivyo hivyo kwa baba, kaka, na mama huongeza kiambiushi /m/ na kuwa mbaba, mkaka na mmama. Haya ni makosa na hatuna budi kujirekebisha.

Tunasoma pia sentensi nyingi hasa kwenye makala zinazoanza na maneno kama lakini na na. Kwa mfano:

“Na hasira, uchungu na ukakasi wa watu hauwezi kuonekana kama nyingine ila kwa njia nyingine.”

“lakini leo viongozi wengi wa Serikali na mashirika ya umma wamekuwa wafanyabiashara wakijipa zabuni kwenye mashirika wanayoongoza wenyewe.”

Kama maneno haya yakiondolewa, maana zake katika sentensi hazitabadilika na zitabaki palepale. Pili, maneno /lakini/ /na/ /na/ ni viunganishi vya vifungu vya maneno ambavyo havijitoshelezi katika maana. Hivyo hatuna haja ya kuyatumia tunapotaka kuanza sentensi.

“Kigoda alisema kuwa dhumuni la uzinduzi wa ofisi hiyo ni kupunguza usumbufu wa gharama kwa wafanyabiashara wanaotaka kuhakiki bidhaa zao.”

Yako maneno ambayo huandikwa kwa katika wingi wake na hayana umoja kama vile, makala, marupurupu, maradhi, madhumuni, maudhi, mahakama, n.k. Mwandishi anapoandika ‘dhumuni la uzinduzi wa ofisi ‘ haina maana kisarufi. Neno madhumuni linabakia kama lilivyo bila kulibadilisha kwa kuondoa kiambishi /ma/ na kubakia dhumuni.

‘Shinikizo hilo likaifanya nchi hiyo ya Rwanda kuacha kujihusisha kuisaidia waasi wa Kongo kwa kuwapatia silaha.”

Imeandikwa kuwa ‘Rwanda kuacha kuisaidia waasi’ ni makosa kisarufi. Ilitakiwa iandikwe ‘…kuacha kuwasaidia waasi.’ Vilevile, ‘kuwapatia silaha’ inasomeka sahihi zaidi kama ingeandikwa ‘kuwapa silaha’. Kwa hiyo, “
Shinikizo hilo likaifanya nchi hiyo ya Rwanda kuacha kuwasaidia waasi wa Kongo kwa kuwapa silaha.”

 

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s