KISWAHILI KINAHIFADHI UMOJA WA UTU WETU BINADAMU

Na Pete Mhunzi

Mengi yameandikwa juu ya thamani ya Kiswahili katika mawasiliano yanayotokea Tanzania kwanza halafu Afrika Mashariki. Makala hii ina shabaha kueleza umuhimu wa hekima inayounganisha watu wote nayo asili yake ni lugha za Kibantu mbali na historia ya Kiingereza lugha ambayo hutambulisha watu kwa rangi na kuwatengisha. Nilisukumwa kuandika makala hii baada ya kusoma makala tano: Ya kwanza ilkuwa Kasumba ya lugha za kigeni inavyoathiri maandiko ya Kiswahili na Stephen Maina 24/08/2012; ya pili Kudumisha Kiswahili ni kudumisha utamaduni wetu na Maggid Mjengwa 02/09/2012; ya tatu, Fasihi ya Kiswahili ikitumika vyema, kwa wakati, itasaidia kujenga maadili na Gadi Solomon 07/12/2012; ya tano, T.V. Redio zifundishe Kiswahili watangazaji wao na Stephen Maina 23/06/2014; zote hizo zilichapishwa katika gazeti la MWANANCHI. Ya mwisho inapatikana katika kijarida cha PAMBAZUKA, toleo ya tarehe 18, mwezi wa sita, mwaka huu nayo mwandishi wake ni Hanno Brankamp. Rwanda: To what extent did the Hamitic myth prepare the ground for 1994?
Makala hizo nne za kwanza zinadhihirisha uwezo na wajibu wa Kiswahili kujenga maadili. Ile ya mwisho inafungua mlango wa mizizi ya ubaguzi katika lugha za magharibi jinsi lugha hizo haswa Kiingereza na Kifaransa zinazojaribu kutumia sayansi na historia kutetea, zaidi kuhalalisha nadharia zinazobainisha ukamilifu kwa uduni wa binadamu unaotambulika katika rangi za ngozi.
Ni nia yangu kupinga kwa nguvu zangu zote utu wangu mzima, matumizi ya maneno “watu weusi na watu weupe nikisisitiza mawazo yanayoleta dhana ya matumizi hayo hauna msingi katika lugha yoyote ya Abantu, huenda lugha zinginezo za Kiafrika mbali na za Kibantu; dhana hiyo ndiyo ni ya Kiingereza. Asili yake inapatikana katika lugha ya Kireno, “negro”. Matumizi yake katika Kireno yalianzia katika uvamizi wa Afrika na matokeo yake: utumwa wa Waafrika.
Ili kujitenga mbali na wazo la kuwa mimi ninatoa maoni yangu yasiyo na msingi katika hekima au falsafa ya Waingereza hebu niwafungulie kamusi ya Standard English-Swahili Dictionary, Oxford University Press 1939 Mhariri: Frederick Johnson.
Katika hicho, neno “race” linatafsiriwa kwa Kiswahili kubeba maana ya “taifa”. Tanzania ni taifa. Wako Waafrika ambao ni Watanzania, pamoja na Wazungu, Wahindi, Wachina, mtu anayetoka kila pembe ya dunia anaweza kuomba uraia nchini Tanzania, mbali na rangi ya ngozi yake. Sasa kile kinachofuatana nacho kinaitwa Standard Swahili-English Dictionary, Oxford University Press, 1939 Mhariri: F. Johnson. Je, tukitafuta neno “taifa” na tafsiri yake kwa Kiingereza tutasoma “race”? Hapana! Maana hiyo ya ubaguzi haipo!
Sasa ninauliza je, kwa nini wataalamu wa lugha viongozi wa Inter-territorial Language (Swahili) Committee (Kamati ya kimaeneo ya lugha ya Kiswahili) Katibu Mkuu alikuwa Frederick Johnson, wangekubaliana na kupata muafaka juu ya tafsiri hiyo ya neno “taifa”isiyo na msingi katika uundaji wa taifa, iwe tafsiri rasmi! Kabla ya kutoa maoni yangu niongeze kauli hiyo na jambo lenye kudhihirisha nia yao. Nayo ni wanachama wote wa kamati kuanzia mnamo mwaka 1930 hadi 1938 walikuwa Waingereza. Wote! Hapakuwa na Mswahili hata mmoja.
Katika kamati iliyokuwa na jukumu la kusanifisha Kiswahili hapana Mswahili!
Tafadhali msomaji mpendwa wangu, usikosi kuliweka maanani ya kuwa mhariri wa kamusi zote mbili zilizotajwa juu ni katibu mkuu wa kamati ile iliyotajwa juu, naye ni Frederick Johnson.
Maoni yangu, jawabu langu la swali langu ni kusema ya kwamba, katika falsafa ya ukoloni na utumwa, wenjeji, wananchi wa Afrika pamoja na Marekani hawana haki ya umiliki wa ardhi. Kwa hivyo serikali zao hazina maana, muundo wa jamii hauna maana, desturi na mila hazina maana. Lugha za ukoloni zinatumika kuwajumlisha wawe bidhaa wasio na jinsi au haki kujitambulisha ila kwa jina waliopewa na Wakoloni nalo ni watu weusi. Tusije kusahau huko Afrika Kusini enzi za Wabeberu ilikuwa marufuku kijinai, kwa mwananchi, mtu mweusi kujiita Mwafrika.
Kwa hivyo ni ufafanuzi wangu kusema neno taifa lilijiwa katika hali ya unafiki likikusudiwa tafsiri katika lugha ya Kiingereza kuthibitisha ukoloni kutokana na majadiliano ya kamati.
Sasa tunaona mfano halisi ya mizizi ya ubaguzi, asili yake na uduni wake. Katika hekima ya Abantu hakuna dhana ya kuwatambulisha watu kutokana na rangi ya ngozi yao.
Mfano wa pili ni historia ya neno “Wazungu”. Ninavyofahamu mimi ni asili yake ni neno zunguka. Wale Waingereza wa kwanza kuingia Afrika Mashariki wanaitwa “explorers” katika Kiingereza. Wao katika matembezi yao ya ugunduzi walionekana machoni mwa wananchi kana kwamba wanazunguka zunguka bure! Wakaitwa Wazungu kutokana na matembezi ambayo yalileta maswali: “Wanafanya nini? Watoto wao, wake zao, nani anawaangalia?” Rangi ya ngozi zao haikuathiri taswira iliyoleta utungaji wa jina Wazungu. Maana yake inatokea na vitendo na jinsi vitendo vilivyofasiriwa na watu waliowaona wageni hao kwa mara ya kwanza.
Mfano wangu wa tatu ni neno “kabila”. Tafsiri yake kwa Kiingereza ni “tribe”. Nimezoea kulisikia neno hili katika mafundisho ya historia ya wananc hi wa asili wa Marekani ambao kutokana na kosa la Nahodha Christopher Columbus, mtu wa kwanza kutoka Ulaya kufika mabara ya Marekani aliyedhani alifika Uhindi kutokana na rangi ya ngozi zao Wahindi kufanana na ile ya wananchi wa asili wa Marekani.
Kosa lilikuwa kuwaita “Wahindi” na mpaka leo hii bado wanaitwa “Wahindi” isipokuwa nchini Kanada ambako wanaitwa watu wa asili= “indigenous people”. Katika Kiingereza cha Afrika ya Mashariki wanaitwa “Wahindi Wekundu” wasije kuchanganywa na Wahindi wenyewe. Baada ya kuanza kusoma historia na matukio ya hivi karibuni katika Afrika neno hilo liliibuka upya. Nikaanza kuona msingi wa matumizi yake katika Kiingereza ama kuwaeleza wananchi wa Marekani au wananchi wa Afrika, ni kuwatambulisha wananchi wa asili wa mabara hayo mawili kuwa watu duni wasio na haki ya umiliki wa ardhi. Wamezaliwa kusibiri ukoloni na utumwa. Wamezaliwa washenzi wanaotangatanga ovyo ovyo mwenendo wayawaya wakiongozwa na wachawi; mbali na watu wa ufalme za Ulaya. Sisi tulifundishwa historia ya Ulaya kwa kuanzia na ufalme halafu mataifa angalau kulikuwa na makabila Ulaya pamoja na kila sehemu nyingine ya dunia.
Ni muhimu sana kudhihirisha thamani ya Kiswahili na uwezo wake kuunganisha watu badala ya kuwatenganisha kama Kiingereza kinavyowatenda .
Inasikitika kusoma na kusikia viongozi pamoja na wadau Watanzania wakitetea Kiswahili na matumizi yake kwa kusema “wengine hawajui Kiingereza.” Je, wanalenga taifa la aina gani? Wanajiona wenye vipaji gani kwa masilahi ya dunia nzima? Watafundisha nini ? Au watabaki wanafunzi, wapokeaji, walaji ambao hawajui kupika? Wakati wa mlo kwao, kitu gani kimeandaliwa katika sahani isipokuwa mdebwede dabwadabwa? Hakuna hata kionjo cha mahanjumati; ladha hakuna! Lishe hakuna!
Tafadhalini jitazame rohoni, moyoni, akilini ambamo hazina ya utu inasubiri kuibuka na kunufaisha watu wote dunia nzima. Asanteni

Advertisements

One thought on “KISWAHILI KINAHIFADHI UMOJA WA UTU WETU BINADAMU

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s