KUDUMISHA KISWAHILI NI KUDUMISHA UTAMADUNI WETU

Maggid Mjengwa

MWANANCHI, Tarehe 02 Mwezi wa Tisa 2012
Maggid Mjengwa
NDUGU zangu,
Juhudi zozote zile za kuitangaza, kuikuza na kuilinda lugha yetu ya Kiswahili ni juhudi za kuulinda utamaduni wetu. Hakika, inahusu utamaduni wetu.
Na utamaduni ni utaratibu wa maisha ikiwa ni pamoja na sanaa za maonesho, muziki asilia, ngoma za asili, tamthilia, lugha, sanaa za ufundi, filamu na chakula. Utamaduni ni utambulisho wa mtu husika.
Tuna kila sababu ya kujikita katika kurejesha heshima, hadhi, moyo na juhudi za kukuza utamaduni wetu ulio kwenye hatari kumezwa na tamaduni za kigeni hususan zile za kimagharibi.
Tutumie utandawazi unaoambatana na sayansi na teknolojia kama nyenzo na fursa ya mafanikio ya jitihada za kuendeleza, kukuza, kusambaza na kuuza utamaduni wetu.Tuuthamini, kuuendeleza na kuukuza utamaduni wetu.
Leo hii ukiangalia muziki unaopigwa kwenye redio zetu, filamu zinazonyeshwa na hata kuigizwa na Watanzania wenzetu.
Ukiangalia namna ya mavazi tunayovaa, vyakula tunavyokula, hata lugha tunayozungumza, vyote hivyo havitoi taswira ya utamaduni halisi wa Mtanzania. Maeneo ya mijini ndiyo yanayoelekea kumezwa zaidi na tamaduni za kighaibu.
Tuna lazima ya kutafakari kwa kina juu ya utamaduni tunaoujenga sasa. Itakumbukwa, miaka ile ya mwanzoni mwa uhuru wetu, masuala ya utamaduni yaliwekwa chini ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Wizara hii ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1962.
Kunako Desemba 10, mwaka 1962, Mwalimu Nyerere aliweka bayana majukumu ya Wizara ya Utamaduni wa Taifa na Vijana.
Mwalimu alitamka yafuatayo, ” Mabadiliko makubwa niliyoyafanya ni kuanzisha wizara mpya ya Utamaduni wa Taifa na Vijana. Nimefanya hivyo kwa kuamini kuwa Utamaduni ni kitu muhimu na ni roho ya taifa lolote liwalo.

Taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu walikosa ari na moyo wenye kuwafanya kuwa taifa.
Moja ya dhambi kubwa ya wakoloni ni ile hali ya kutufanya tuamini kuwa hatuna utamaduni wetu wa asili au kwamba yote tuliyokuwa nayo hayakuwa na thamani yeyote, kitu ambacho tulipaswa tukionee aibu, badala ya kuwa chanzo cha kujivunia.
Baadhi yetu, hasa wale tulioelimishwa na Wazungu tunajaribu kuwathibitishia wakoloni waliotutawala kwamba, “tumestaarabika” ikiwa na maana tumeachana na yale yote yenye kutuunganisha na utamaduni wetu wa asili.

Kwamba tumejifunza kuiga utamaduni wa Kizungu. Malengo ya vijana wetu hayakuwa kuwa Waafrika walioelimika bali kuwa Wazungu Weusi.” Hayo ni maneno ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962.
Bila shaka, Mwalimu Nyerere alikuwa ni mfano wa viongozi waliothamini na kuuenzi utamaduni wetu ikiwemo Lugha ya Kiswahili. Leo tunashuhudia jinsi jamii yetu ilivyovamiwa na tamaduni za kigeni. Ni dhahiri kuwa utamaduni unaimarika kwa kuiga yaliyo mazuri kutoka tamaduni nyingine.
Lakini katika jamii yetu, tamaduni za kigeni hususan kutoka Ulaya na Marekani zinaelekea kukumbatiwa zaidi na wanajamii, hivyo kuhatarisha kuufifisha na pengine kuuangamiza utamaduni wetu.

 Vijana wetu wanaona fahari zaidi kuimba na kucheza nyimbo na miziki ya kighaibu. Wanaona aibu kuimba nyimbo za Kiswahili. Nyimbo za makabila yetu kwa mfano Kinyamwezi, Kizaramo na nyinginezo za asili.
Vijana wetu wanaona fahari kuongea Kiswahili kwa lafudhi ya Kiingereza au Kimarekani.
Vijana wetu wengi wa siku hizi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kucheza Gombe Sugu, Mganda, Mangala, Konge, Nyang’umumi, Kiduo, au Lele Mama.

Hizi ni baadhi tu ya ngoma zetu za asili. Vijana wetu wengi hawajawahi kusikia au hata kujaribu kupiga vyombo vya muziki vya asili kama vile Marimba, Kilamzi, Ligombo au Imangala.

Tuangalie ni jinsi gani tutaweza kuuhifadhi, kuuendeleza na kuuimarisha utamaduni wetu.

Labda hapa kuna haja ya pekee ya kutoa mfano wa suala la matumizi ya lugha kwa vile ndiyo kitovu cha utamaduni. Kwa upande wetu ni Lugha ya Kiswahili.
Hivi leo kuna wanaozungumza au kuandika kwa Kiingereza mahali ambapo asilimia 90 ya wasikilizaji au wasomaji ni wazungumzaji wa Kiswahili.

Hiyo ni hali ya kutojiamini. Ni kubaki katika hali ya utumwa wa fikra.
Je, wenye kufanya hivyo, wana malengo ya kuwaonyesha “wakoloni” au “Wafadhili” wa semina kwamba wao “Wamestaarabika”?
Au wanafanya hivyo ili kuwaridhisha wafadhili tu? (Rejea kauli ya Mwalimu Nyerere mwaka 1962 hapo juu).

Kwa nini waandaaji wa semina wasitumie wakalimani kuwatafsiria wasio wazungumzaji wa Kiswahili ambao ni asilimia kumi tu ya kadamnasi?
Hilo pia lingetengeneza ajira kwa baadhi ya Watanzania.
Suala la kujiamini ni suala la utambulisho. Binadamu hawezi kujiamini kama hana hakika ya utambulisho wake. Tujiulize, sisi ni nani?
Hili ni swali gumu na la kifalsafa. Lakini ni swali lenye kuhitaji majibu ili tuweze kujenga msingi imara wa utamaduni wetu.
Nimechokoza mjadala…
0788 111 765, 0754 678 252

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s