MCHANGO WA KIINGEREZA KATIKA KUDUDUMIZA MAENDELEO YA ELIMU NCHINI

 Faraja Kristomus

Faraja Kristomus

Sehemu ya Pili
Katika makala yaliyopita tuliangalia jinsi silabasi yetu ya Kiingereza ya 2005 ilivyo na mambo mengi ambayo endapo yangezingatiwa kwa umakini katika ufundishaji huenda tusingekuwa na tatizo la wanafunzi wa darasa la saba kushindwa kujua Kiingereza wanapohitimu.
Pia tuliona jinsi wizara ya elimu ilivyotenga saa nyingi kwa mwaka kwa ajili ya kufundisha Kiingereza. Haya mambo mawili yangesaidia walau kuwa na wanafunzi wenye kiwango kikubwa cha kuweza kutumia au kuzungumza Kiingereza.
Leo tutazungumzia mbinu za ufundishaji wa lugha hii ya Kiingereza hapa nchini. Lakini kabla ya kupitia mbinu hizo, hebu tuangalie kinadharia jinsi lugha ya Kiingereza ilivyotawanyika duniani. Mtawanyiko huu uko katika ngazi tatu.
Ngazi ya kwanza ya mtawanyiko huo ni kule ambako Kiingereza ni lugha mama. Mfano ni Uingereza, Marekani, Kanada, New Zealand, na Australia. Katika nchi hizi Kiingereza kinafundishwa kama lugha ya kwanza, lugha mama, au lugha ya asili.
Ngazi ya pili ya myawanyiko wa Kiingereza ni kule ambako kinazungumzwa kama lugha ya pili. Hapa namaanisha kuwa watu wanakuwa na lugha zao za kwanza au lugha mama; ambazo mara nyingi ni lugha za makabila yao halafu wanapotoka nje ya makabila yao wanazungumza Kiingereza kama lugha ya taifa au lugha ya kuwaunganisha (lingua franca).
Kiingereza kwa ngazi hii ya pili kilisambazwa kwa njia ya ukoloni, hivyo kinachukuliwa kuwa lugha ya pili katika nchi zile ambazo mkoloni wao alikuwa ni Mwingereza. Mfano ni Kenya, Uganda, Malawi, Zimbabwe, Nigeria, India, Afrika ya Kusini, Ghana, Zambia nk.
Katika nchi hizi, Kiingereza kinapewa umuhimu zaidi kwasababu ni lugha pekee inayowaunganisha wananchi na hivyo ufundishaji wa Kiingereza unatiliwa maanani sana na wanafunzi wanakuwa na motisha ya kujifunza ili waweze kuwa na nafasi ya kwenda popote katika nchi yao na kuweza kuwasiliana.
Katika kundi hili imo Tanzania lakini kutokana na sera yetu ya lugha, Kiswahili kimechukua nafasi ya Kiingereza kama lugha ya kuwaunganisha watanzania na hivyo Kiingereza kwa wengi wetu ni kama lugha ya kigeni. Watanzania wengi wanajifunza lugha ya Kiingereza kama lugha ya tatu baada ya lugha za makabila na Kiswahili.
Ngazi ya tatu ya mtawanyiko wa Kiingereza duniani ni kule ambako Kiingereza kinafundishwa na kuzungumuzwa kama lugha ya kigeni. Katika kundi hili Kiingereza kinapewa umuhimu mkubwa kama lugha ya kimataifa lakini nchi zenyewe hazina uhusiano wa kikoloni na Uingereza. Nchi hizo ambako Kiingereza kinafundishwa kama lugha ya kigeni ni Japan, Ujerumani, Uchina, Korea, Brazil, Israel, Urusi, Ufaransa nk.
Kwa hiyo kwa kuangalia mtawanyiko huo wa Kiingereza duniani, huwezi kutegemea kuwa na mfumo mmoja wa kufundisha Kiingereza duniani kote.
Kwa upande wa Tanzania, sera yetu ya lugha inasema kuwa Kiingereza ni lugha rasmi na itatumika kufundishia kuanzia sekondari hadi vyuo vikuu. Hata hivyo inaonekana wanafunzi wengi wanapata shida sana kujieleza na kuitumia lugha hii wawapo darasani na nje ya darasa.
Hata hivyo bado tunaweza kuamua kukifundisha Kiingereza kwa ufasaha katika ngazi ya shule ya msingi na mwanafunzi anapojiunga sekondari akawa na uwezo wa kumudu masomo.
Mfumo wa ufundishaji Kiingereza nchini Tanzania ni ule wa Kimawasiliano (Communicative Language Teaching – CLT). Muhtasari wa Kiingereza wa mwaka 2005 na ambao unatumika mpaka sasa unaelekeza mwalimu atumie mbinu hii katika kufundisha Kiingereza.
Mbinu hii inatilia mkazo juu ya kuifundisha lugha kama nyenzo ya mawasiliano, na kuachana na mbinu ya kufundisha lugha kwa kusisitiza zaidi juu ya sarufi na msamiati. Mbinu hii inalenga kuwapa wanafunzi ujuzi wa kimawasiliano unaowawezesha kuwa na stadi mbalimbali za kuwasiliana kwa kutumia lugha.
Stadi ambazo mwanafunzi anatakiwa azipate kwa kupitia mbinu hii ni pamoja na kuwa na ujuzi wa lugha (uelewa na uwezo wa kujifunza matamshi, msamiati na sarufi); kujua matumizi ya lugha kulingana na mazingira; kuwa na stadi nne za umahiri wa lugha yaani kusikiliza, kuongea, kusoma na kuandika; na pia kujua matumizi sahihi ya lugha kwa kuendana na muktadha na nyanja tofauti.
Mbinu ya mawasiliano inamtaka mwalimu afundishe Kiingereza kwa Kiingereza. Kinacholengwa katika mbinu hii si usahihi wa lugha bali ufanisi wa mawasiliano. Wanafunzi wanasisitizwa wajifunze kuhusu masuala ya mawasiliano na madhumuni yake (kama vile uandishi wa barua za aina zote, mawasiliano uwanja wa ndege, mazungumzo hotelini nk.).
Msingi wa mfumo huu wa ufundishaji ni kwamba mwalimu anapaswa kutambua mahitaji ya wanafunzi, kukuza uwezo binafsi wa mwanafunzi kujifunza, kuwa mwezeshaji na siyo mdhibiti wa mchakato wa kujifunza, kumpa mwanafunzi hamasa ya kujifunza kwa kumwongoza kwa maneno na matendo. Pia mwalimu anapaswa kubuni njia au kazi mbalimbali zitakazomfanya mwanafunzi ajifunze zaidi.
Mpaka sasa inaonekana kuwa mbinu yetu ya kufundishia Kiingereza si kikwazo cha wanafunzi kujua Kiingereza. Katika makala ya wiki ijayo tutaangalia wapi kuna tatizo na jinsi ya kuweza kutatua tatizo hilo.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s